• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Chipolopolo ya Zambia yaajiri kocha Avram Grant aliyewahi kudhibiti mikoba ya Chelsea, West Ham na Ghana

Chipolopolo ya Zambia yaajiri kocha Avram Grant aliyewahi kudhibiti mikoba ya Chelsea, West Ham na Ghana

NA MASHIRIKA

ZAMBIA wamemteua kocha wa zamani wa Chelsea, West Ham United na Ghana, Avram Grant, kudhibiti mikoba ya timu yao ya taifa almaarufu Chipolopolo.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Zambia (FAZ), Grant ambaye ni mkufunzi raia wa Israel, amekubali mkataba wa miaka miwili.

“Nilikuwa nikisubiri ofa nzuri ya kunoa kikosi ambacho kitaibua ubora wangu katika ulingo wa ukufunzi. Hiyo ndiyo sababu ambayo imenifanya kuteua Zambia,” akasema Grant katika mahojiano yake na wanahabari jijini Lusaka.

“Nilikubali ofa ya kunoa timu ya Zambia kwa sababu naamini ndicho kikosi kitakachonipa changamoto mpya. Wakati wangu wa kuondoka utakapofika, tutatazamia kutathmini kikosi na kufurahia kazi nzuri ambayo tutakuwa tumefanya katika juhudi za kuwekea wanasoka wetu chipukizi msingi thabiti,” akaongezea.

Grant, 67, ana tajriba pevu katika soka ya Afrika ikizingatiwa kuwa aliwahi kuongoza Ghana kutinga fainali ya Kombe la Afrika (AFCON) mnamo 2015 ila masogora wake wakazidiwa maarifa na Ivory Coast kupitia penalti. Alijiuzulu kambini mwa Ghana mnamo 2017 baada ya kikosi chake kuambulia nafasi ya nne kwenye fainali za AFCON.

Grant ambaye amedhibiti mikoba ya vikosi kadhaa nchini Israel, Uingereza na Serbia, anajaza nafasi ya mwanasoka wa zamani wa Zambia, Moses Sichone, ambaye amekuwa akishikilia mikoba ya Chipolopolo tangu mkufunzi raia wa Croatia, Aljosa Asanovic, aagane na Zambia mnamo Septemba 2022. Sichone anatarajiwa kudumisha wadhifa wake wa kocha msaidizi.

Kubwa zaidi katika malengo ya Grant ni kufufua makali ya Zambia waliotawazwa wafalme wa AFCON 2012. Chipolopolo hawakufuzu kwa fainali za makala ya kipute hicho mwaka huu nchini Cameroon na wakaambulia nafasi ya tatu katika kundi lao la kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022.

Zambia wanajivunia chipukizi wengi wa haiba kubwa akiwemo fowadi matata wa Rangers, Fashion Sakala, na mshambuliaji wa Leicester City, Patson Daka, aliyeongoza chipukizi wa Zambia U-20 kujizolea ufalme wa AFCON 2017 kabla ya kutinga robo-fainali za Kombe la Dunia baadaye mwaka huo.

Pambano la kwanza litakalotandazwa na Zambia chini ya Grant ni dhidi ya Lesotho mnamo Machi 2023 kwa ajili ya kufuzu kwa fainali za AFCON 2023 nchini Ivory Coast.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

  • Tags

You can share this post!

Washukiwa watatu wakamatwa kwa kuiba mali ya Kenya Power...

Feri kuanza kutembeza watalii ndani ya bahari

T L