• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Dalili kocha Ronald Koeman atapigwa kalamu na Barcelona mwishoni mwa msimu huu

Dalili kocha Ronald Koeman atapigwa kalamu na Barcelona mwishoni mwa msimu huu

Na MASHIRIKA

KOCHA Ronald Koeman amedai kwamba haheshimiwi na vyombo vya habari pamoja na vinara wa bodi ya Barcelona huku tetesi kuhusu uwezekano wa kutimuliwa kwake ugani Camp Nou zikizidi kushika kasi.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, kiungo wa zamani wa Barcelona Xavi Hernandez anatarajiwa kurithi mikoba ambayo Koeman atapokonywa na Barcelona mwishoni mwa msimu huu.

Mustakabali wa Koeman uwanjani Camp Nou unaanza kumulikwa siku chache baada ya rais mpya wa Barcelona Joan Laporta kukiri kwamba kutakuwepo na mabadiliko makubwa muhimu kambini mwa kikosi hicho mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21.

“Watu wanastahili kuheshimu kocha pamoja na wachezaji wao. Katika siku za mwisho za kampeni za msimu huu, sijahisi kabisa kwamba usimamizi wa Barcelona unaniunga mkono,” akatanguliza Koeman.

“Vyombo vya habari vinaibuka na madai mapya kila siku na usimamizi umesalia kimya kuhusu baadhi ya madai hayo. Sijajua kiini cha matukio hayo. Lakini nimetambua kwamba hapa Uhispania, kuna mazoea ya vyombo vya habari kujihusisha sana na mustakabali wa kocha wa kikosi chochote. Hilo ni jambo ambalo nahisi kwamba ni utovu wa heshima,” akaongeza Koeman ambaye ni raia wa Uholanzi.

Koeman ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Everton, aliajiriwa na Barcelona mnamo Agosti 2020 kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kujiuzulu kambini mwa Uholanzi. Kuajiriwa kwake kulitokana na tukio la kutimuliwa kwa mkufunzi Quique Setien.

Licha ya Koeman kushindia Barcelona taji la Copa del Rey mnamo Aprili 2021, miamba hao wamesuasua pakubwa katika mechi kadhaa zilizopita na kwa utepetevu huo ukawanyima fursa ya kujitwalia taji la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu.

Barcelona kwa sasa watakamilisha kampeni za La Liga nje ya nafasi ya mbili-bora kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2007-08.

Aidha, kikosi hicho kilibanduliwa na Paris Saint-Germain (PSG) ya Uhispania kwenye hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu huku nyota tegemeo Lionel Messi akiwa bado hajarefusha mkataba wake ugani Camp Nou.

Alipoulizwa kuhusu mustakabali wake ugani Camp Nou, Koeman alisema: “Kwa kweli sioni uwezekano wowote wa kuendelea kwangu kuhudumu kambini mwa Barcelona. Hapana haja kuendelea kukaa mahali ambapo huheshimiwi japo sijazungumza na rais mpya wa klabu kuhusiana na suala hilo.”

“Najua mabadiliko ni muhimu na ni jambo la lazima kwa Barcelona kufanya iwapo watataka kuanza tena kujishindia mataji. Ikiwa mabadiliko hayo yatakuwa kwa upande wa wachezaji au benchi ya kiufundi, basi ni sawa kabisa ila ni muhimu kwa wahusika kutangaziwa maamuzi hayo ya bodi mapema,” akaongeza Koeman.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo, Laporta hana imani kubwa na Koeman wala Hernandez kuwa kocha wa Barcelona na amedokeza uwezekano wa kikosi hicho kuajiri ama Hansi Flick wa Bayern Munich au aliyekuwa mchezaji wa Barcelona, Frank Rijkaard.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ureno wafichua kikosi cha wanasoka 26 watakaotegemewa...

Manchester United wathibitisha kuwa jeraha litamkosesha...