• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 AM
Manchester United wathibitisha kuwa jeraha litamkosesha beki Maguire fainali ya Europa League dhidi ya Villarreal

Manchester United wathibitisha kuwa jeraha litamkosesha beki Maguire fainali ya Europa League dhidi ya Villarreal

Na MASHIRIKA

KOCHA Ole Gunnar Solskjaer wa Manchester United amesema kwamba beki na nahodha Harry Maguire hatakuwa sehemu ya kikosi atakachokitegemea dhidi ya Villarreal kwenye fainali ya Europa League itakayowakutanisha mjini Gdansk, Poland mnamo Mei 26, 2021.

Maguire ambaye ni raia wa Uingereza, alipata jeraha la kifundo cha mguu ambalo litamnyima uhondo wa fainali hiyo wakati alipokuwa akichezea Man-United dhidi ya Aston Villa mnamo Mei 9, 2021 uwanjani Villa Park.

Beki huyo alihudhuria hafla ya kufyatuliwa kwa filamu kumhusu kocha Sir Alex Ferguson uwanjani Old Trafford mnamo Alhamisi ya Mei 20 bila ya mikongojo ambayo amekuwa akitembelea tangu apate jeraha.

Tukio hilo liliibua tetesi kuhusu iwapo amepona kiasi cha kutegemewa na Man-United dhidi ya Villarreal inayotiwa makali na kocha wa zamani wa Arsenal, Unai Emery.

“Anatembea sasa bila usaidizi wa mikongojo. Lakini angali na safari ndefu ya kupona. Bado hawezi kukimbia na hajaanza hata kushiriki mazoezi mepesi uwanjani,” akatanguliza Solskjaer.

Sidhani mashabiki watakuwa na fursa ya kumtazama akicheza uwanjani jijini Gdansk. Aliumia vibaya na atahitaji muda zaidi,” akasema kocha huyo raia wa Norway kwa kudokeza uwezekano wa Maguire kukosa pia fursa ya kuchezea Uingereza kwenye fainali zijazo za Euro kati ya Juni 11 na Julai 11, 2021.

Kwa mujibu wa Solskjaer, Maguire atakuwa sehemu ya kikosi kitakachofunga safari ya kuelekea Poland kwa fainali ya Europa League hata kama hatachezeshwa.

Mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) watapania kutumia fainali hiyo kutia kapuni taji lao la kwanza tangu 2017 na watafunga rasmi kampeni za EPL muhula huu dhidi ya Wolves uwanjani Molineux mnamo Mei 23, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Dalili kocha Ronald Koeman atapigwa kalamu na Barcelona...

Uweza Women yawapa akina dada jukwaa la matumaini kukuza...