• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Depay anaogelea kwenye bahari ya manoti Camp Nou

Depay anaogelea kwenye bahari ya manoti Camp Nou

Na CHRIS ADUNGO

MEMPHIS Depay, 27, ni mwanasoka raia wa Uholanzi ambaye sasa ni fowadi tegemeo kambini mwa Barcelona, katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Alianza kutandaza soka ya kulipwa akivalia jezi ya PSV Eindhoven katika Ligi Kuu ya Uholanzi (Eredivisie) chini ya kocha Philip Cocu, aliyemwajibisha katika michuano karibu yote ya kikosi cha kwanza.

Depay alifunga mabao 50 kwenye mechi 124 alizochezea PSV katika mashindano yote, na kutawazwa mfungaji bora wa Eredivisie mnamo 2014-15 akiwa amepachika wavuni magoli 22 katika mechi 30.

Aliongoza waajiri wake hao kutwaa taji la Eredivisie kwa mara ya kwanza mnamo 2008, na akaibuka Mwanasoka Bora wa Mwaka kufuatia matokeo bora ya muhula huo.Shirikisho la Soka la Ufaransa lilimtawaza Depay kuwa Chipukizi Bora wa Mwaka 2015 kwa matokeo ya kuridhisha uwanjani.

Depay alijiunga na Manchester United ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Juni 2015 kwa kima cha Sh3.9 bilioni.Baada ya nyota yake kutong’aa ugani Old Trafford, fowadi huyo aliyoyomea Ufaransa kuvalia jezi ya Olympique Lyon mnamo Januari 2017.

Alihudumu huko kwa misimu minne kabla kusajiliwa na Barca mnamo 2021.Depay amewakilisha Uholanzi katika mashindano ya viwango mbalimbali. Alikuwa sehemu ya kikosi cha U-17 kilichoshinda taji la Euro 2011.

Aliwajibishwa kwa mara ya kwanza katika timu ya watu wazima mnamo 2013, kabla ya kuongoza taifa lake kuambulia nafasi ya tatu kwenye Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.Tangu wakati huo, ameunga kikosi cha kwanza na kuwajibishwa dimba la Euro 2020.

UKWASIKwa mujibu wa majarida ya Forbes na Celebrity, thamani ya mali ya Depay inakadiriwa kufikia kima cha Sh5 bilioni.Kiini kikubwa cha ukwasi wake ni mshahara wa Sh20 milioni aliokuwa akipokezwa kila wiki na Lyon, kabla Barcelona kunyakua huduma zake kwa Sh39 milioni kwa wiki.

Mbali na ujira huo mnono, Depay pia hujirinia fedha za ziada kutokana na dili za matangazo na marupurupu ya kushinda mechi.Kwa ufupi, yeye hutia mfukoni zaidi ya Sh3 bilioni kila mwaka.? Kiasi hicho cha fedha kinamweka nyuma ya nyota Sergio Aguero, Sergio Busquets na Frenkie de Jong ambao sasa wanadumishwa na Barca kwa mishahara ya juu zaidi katika soka ya Uhispania, tangu Lionel Messi aondoke kuelekea Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Depay alifichua kwamba yeye hutumiwa sana na jarida la Netherlands FIFA Edition kutangaza bidhaa za kampuni ya Nike, ambayo humpokeza takriban Sh40 milioni kila mwezi.

Depay pia ni balozi wa kutangaza bidhaa za kampuni ya Electronic Arts (EA Sports) inayomlipa kima cha Sh28 milioni kila mwezi.MAGARIJapo Depay anamiliki magari mengi ya haiba, anayoyapenda zaidi ni Ferrari 458, Bentley Continental GT, Mercedes-Benz AMG-GTR Coupe na 918 Spyder yaliyomgharimu Sh98 milioni.

MAKASRI Zaidi ya kumiliki jumba la kibiashara la Sh680 milioni nchini Uholanzi, moja kati ya mawili ya kifahari anayojivunia mjini Moordrecht nchini humo ni lile la Sh500 milioni, alilowajengea wazazi wake Dennis na Cora Schensema mnamo 2018. Kwa sasa anaishi katika jumba la Sh440 milioni kule Uhispania.

FAMILIA NA MAPENZI Depay alizaliwa mjini Moordrecht mnamo Februari 13, 1994.Fowadi huyo mraibu wa kuchanja chale mwilini, sasa hana mchumba baada ya mrembo Lori Harvey – aliyekuwa akimburudisha kimapenzi tangu Juni 2017 – kutemana naye mwanzoni mwa mwaka huu.Lori ndiye kitinda mimba katika familia ya mwendeshaji vipindi maarufu za runinga nchini Amerika, Steve Harvey.

You can share this post!

Waziri asema wauguzi hawakufeli mtihani

Kaunti ya Nairobi yaanzisha mfumo mpya wa kulipia huduma

T L