• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Depay na Wijnaldum waongoza Uholanzi kuzima ndoto ya Macedonia kwenye Euro

Depay na Wijnaldum waongoza Uholanzi kuzima ndoto ya Macedonia kwenye Euro

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

MABAO kutoka kwa Memphis Depay na Georginio Wijnaldum yalisaidia Uholanzi kupepeta Macedonia Kaskazini 3-0 na kukamilisha kampeni zao za Kundi C bila kupoteza hata mechi moja.

Mechi hiyo ilihudhuriwa na mashabiki 12,000 uwanjani Johan Cruyff Arena jijini Amsterdam, Uholanzi. Chini ya mkufunzi Frank de Boer, Uholanzi walijibwaga ugani kuvaana na Macedonia mnamo Jumatatu wakiwa tayari wamefuzu kwa hatua ya 16-bora baada ya kuchabanga Ukraine na Austria kwenye michuano miwili ya ufunguzi.

Depay ambaye sasa ni mali rasmi ya Barcelona, aliwafungulia Uholanzi ukurasa wa mabao katika dakika ya 24 baada ya kushirikiana vilivyo na beki Daley Blind. Mabao mengine ya Uholanzi yalifumwa wavuni na Wijnaldum ambaye ni sajili mpya wa Paris Saint-Germain (PSG) katika dakika za 51 na 58.

Depay kwa sasa anajivunia mabao tisa na amechangia matatu mengine kutokana na mechi 10 zilizopita ndani ya jezi za Uholanzi. Uholanzi kwa sasa wataelekea jijini Budapest, Hungary mnamo Juni 27 kwa ajili ya mchuano wao wa hatua ya 16-bora ambapo watamenyana na kikosi kitakachoambulia nafasi ya tatu kutoka Kundi D, E au F.

Mechi kati ya Macedonia na Uholanzi ilimpa nahodha Goran Pandev wa Macedonia fursa ya kuchezea taifa lake kwa mara ya 122 ambayo ilikuwa ya mwisho kabla ya kuangika rasmi daluga zake kwenye soka ya kimataifa.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 37 anastaafu soka akishikilia rekodi ya mchezaji ambaye amewajibishwa na timu ya taifa mara nyingi zaidi na aliyefunga mabao mengi zaidi (38). Wakishiriki fainali za Euro kwa mara ya kwanza mwaka huu, Macedonia Kaskazini ndiyo timu ya kwanza kubanduliwa kwenye kampeni za Euro baada ya kupigwa na Austria na Ukraine katika michuano miwili ya kwanza kwenye Kundi C.

Macedonia Kaskazini ndiyo timu ya nne kuwahi kupoteza mechi zote tatu wakishiriki fainali za Euro kwa mara ya kwanza. Uturuki waliwahi kufanya hivyo mnamo 1996 baada ya Denmark (1964) na Ufaransa mnamo 1960.

 

  • Tags

You can share this post!

Ubelgiji wapepeta Finland kirahisi na kujikatia tiketi ya...

Austria waingia hatua ya 16-bora ya Euro kwa mara ya kwanza...