• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 11:46 AM
Ubelgiji wapepeta Finland kirahisi na kujikatia tiketi ya 16-bora kwenye Euro

Ubelgiji wapepeta Finland kirahisi na kujikatia tiketi ya 16-bora kwenye Euro

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

UBELGIJI waliendeleza ubabe wao kwenye kampeni za Euro mwaka huu kwa kuwapiga Finland 2-0 katika mchuano wa Kundi B mnamo Jumatatu usiku jijini St Petersburg, Urusi.

Ni mara ya kwanza kwa Ubelgiji kuwahi kushinda mechi zote tatu za hatua ya makundi kwenye fainali za Euro.Kikosi hicho kinachoorodheshwa na FIFA katika nafasi ya kwanza duniani, kilifungiwa mabao na kipa Lukas Hradecky aliyejifunga katika dakika ya 74 kabla ya Romelu Lukaku kucheka na nyavu za Finland dakika saba baadaye.

Ushindi wa Ubelgiji ulishuhudia Finland wakishuka hadi nafasi ya tatu kundini kwa alama tatu baada ya Denmark kusajili ushindi mnono wa 4-1 dhidi ya Urusi jijini Copenhagen. Finland wanalazimika sasa kusubiri iwapo watakuwa miongoni mwa timu nne zitakazobahatika kusonga mbele baada ya kusajili matokeo ya kuridhisha na kuambulia nafasi za tatu kwenye makundi yao.

Kwa upande wao, Denmark watamenyana sasa na Wales kwenye hatua ya 16-bora mnamo Juni 26 jijini Amsterdam, Uholanzi.Kufikia sasa, vikosi ambavyo vipo pazuri zaidi kusonga mbele baada ya kusajili matokeo ya kuridhisha na kukamilisha kampeni zao za makundi katika nafasi za tatu ni Uswisi na Ukraine.

Ushindi wa Ubelgiji dhidi ya Finland unaamanisha kwamba Uingereza, Jamhuri ya Czech, Uswidi na Ufaransa bado watasonga mbele kwa hatua ya 16-bora hata iwapo watakamilisha kampeni zao katika nafasi za tatu makundini kwa sababu tayari wana alama alama nne kila mmoja.

Ubelgiji watachuana na mojawapo ya timu zitakazoambulia nafasi za tatu makundini mnamo Juni 27 jijini Sevilla, Uhispania. Chini ya kocha Roberto Martinez, Ubelgiji wanapigiwa upatu wa kunyanyua taji la Euro ikizingatiwa kwamba wamepoteza mechi moja pekee kutokana na 26 zilizopita.

 

  • Tags

You can share this post!

Denmark kumenyana na Wales kwenye muondoano wa Euro

Depay na Wijnaldum waongoza Uholanzi kuzima ndoto ya...