• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Difenda Kieran Gibbs wa West Brom kuyoyomea Amerika kuchezea Inter Miami mwisho wa msimu huu

Difenda Kieran Gibbs wa West Brom kuyoyomea Amerika kuchezea Inter Miami mwisho wa msimu huu

Na MASHIRIKA

BEKI wa zamani wa Arsenal, Kieran Gibbs, 31, ataingia katika rasmi ya kikosi cha Inter Miami kinachomilikiwa na jagina wa soka David Beckham nchini Amerika baada ya mkataba wake na West Bromwich Albion ya Uingereza kutamatika mwishoni mwa msimu huu.

Gibbs atakuwa mchezaji wa pili mwaka huu kutoka soka ya Uingereza baada ya aliyekuwa nahodha wa Stoke City, Ryan Shawcross, kuingia katika kikosi cha Inter Miami kinachoshiriki Major League Soccer (MLS)

Gibbs ambaye ni raia wa Uingereza, alisajiliwa na West Brom mnamo 2017 baada ya kuvalia jezi za Arsenal kwa kipindi cha miaka 10. Ushawishi wake uwanjani The Hawthorns ulichangia kupandishwa daraja kwa kikosi cha West Brom hadi Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mwishoni mwa msimu wa 2019-20.

Hata hivyo, amechezeshwa na kocha Sam Allardyce wa West Brom katika mechi 11 pekee za EPL msimu huu, mara ya mwisho ikiwa katika mechi iliyowashuhudia wakiambulia sare ya 2-2 dhidi ya Fulham mnamo Januari 30, 2021.

West Brom kwa sasa wanashikilia nafasi ya 19 kwenye msimamo wa jedwali la EPL na wako katika hatari ya kushushwa daraja pamoja na Fulham na Sheffield United wanaovuta mkia.

Kwa upande wao, Inter Miami walikamilisha kampeni zao za soka ya MLS katika nafasi ya 10 mnamo 2020 na kwa sasa wanajiandaa kwa msimu mpya utakaoanza Aprili 2021 na kukamilika Disemba 2021. Huu utakuwa msimu wao wa pili kwenye kivumbi cha MLS.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Pigo kwa Chelsea na PSG baada ya beki David Alaba kufichua...

Sheria mpya za unywaji pombe Kiambu