• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Pigo kwa Chelsea na PSG baada ya beki David Alaba kufichua kwamba mpango wake ni kutua Barcelona au Real Madrid

Pigo kwa Chelsea na PSG baada ya beki David Alaba kufichua kwamba mpango wake ni kutua Barcelona au Real Madrid

Na MASHIRIKA

NDOTO ya Chelsea kujivunia huduma za beki David Alaba atakayeagana rasmi na Bayern Munich ya Ujerumani mwishoni mwa msimu huu imezimika.

Hii ni baada ya mwanasoka huyo raia wa Austria kufichua kwamba azma yake ni kuyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Real Madrid au Barcelona.

Mkataba kati ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 na Bayern unatamatika mwishoni mwa muhula huu wa 2020-21 na Alaba hayuko radhi kutia saini mkataba mpya uwanjani Allianz Arena.

Ingawa yalikua matamanio ya kocha Thomas Tuchel kumshawishi Alaba kutua uwanjani Stamford Bridge, vinara wa Chelsea wamefichua ugumu wa kumdumisha beki huyo kimshahara ikizingatiwa kwamba analenga kulipwa Sh54 milioni kwa wiki.

Kwa mujibu wa gazeti la Sky nchini Ujerumani, Alaba ametupilia mbali ofa nyingine ya kujiunga na Paris Saint-Germain (PSG) walikuwa radhi kumpokeza ujira wa Sh30 milioni kwa wiki uwanjani Parc des Princes, Ufaransa.

Real ya kocha Zinedine Zidane tayari imefichua azma ya kumlipa Alaba mshahara wa Sh2.3 bilioni kwa mwaka, jambo ambalo linatarajiwa kumpa msukumo wa kutua uwanjani Santiago Bernabeu badala ya Camp Nou, Barcelona.

Alaba kwa sasa ndiye mchezaji wa sita ghali zaidi kambini mwa Bayern baada ya Robert Lewandowski, Manuel Neuer, Thomas Muller, Lucas Hernandez na Jerome Boateng. Tangu awajibishwe na Bayern kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 17 mnamo Februari 2010, amewaongoza miamba hao kutia kapuni mataji tisa ya Bundesliga na sita ya German Cup.

Alaba ametawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka nchini Austria mara saba na alitwaa tuzo hiyo mara sita mfululizo kati ya 2011 na 2016.

Tangu avalie jezi ya timu ya taifa ya Austria kwa mara ya kwanza mnamo 2009 akiwa na umri wa miaka 17 pekee, Alaba amechezea kikosi hicho katika zaidi ya mechi 70 na alikuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa na Austria kwenye fainali za Euro 2016 nchini Ufaransa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

NDONDI: Ratiba ya awamu ya tatu ya Africa Zone 3

Difenda Kieran Gibbs wa West Brom kuyoyomea Amerika...