• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 9:50 AM
Dkt Ahmed Kalebi awapa motisha Gogo Boys kujitahidi zaidi msimu huu

Dkt Ahmed Kalebi awapa motisha Gogo Boys kujitahidi zaidi msimu huu

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya Gogo Boys imeibuka kati ya vikosi vinavyoendelea kutesa sio haba katika soka la viwango vya mashinani hasa eneo bunge la Kibra, Kaunti ya Nairobi.

Mlezi wa klabu hiyo aliye bosi wa kampuni ya Lancet, Dkt Ahmed Kalebi anasema kuwa wanasoka hao wamepania kufanya kweli na kufuzu kushiriki soka la ligi ya hadhi ya juu nchini ndani ya muda mchache ujao.

”Bila kuwapigia debe wanasoka wa Gogo Boys wanazidi kufanya vizuri hali inayoashiria kuwa wanalenga kuibuka kati ya timu mahiri nchini,” bosi huyo alisema na kutoa wito kwao kutolegeza kamba dimbani.

Licha ya michezo ya vipute mbali mbali kusitishwa kutokana na mlipuko wa virusi vya corona, Gogo Boys yenye makazi yake katika mtaa wa Kibera imekuwa ikifanya vizuri kwenye mechi za mashindano tofauti. Kikosi hicho kinajivunia kufanya vizuri kwenye mashindano ya mataji mawili ndani ya miezi minne iliyopita baada ya mechi za ligi zote kupigwa stopu mwezi Machi 2020.

Wachana nyavu hao wa kocha, Wilberforce Chisira walibeba taji la Kriss Darlin Super Cup wiki iliyopita walipozaba Ping FC kwa mabao 2-1 katika fainali iliyopigiwa Uwanjani Woodley Kibra, Nairobi.

Vijana hao walitawazwa mabingwa wa kombe hilo huku wakijivunia kumaliza katika nafasi ya pili kwenye mashindano ya Slum Championship. Katika ngarambe iliyotangulia ya Slum Champions wapigagozi hao walimaliza nafasi ya pili baada ya kulimwa mabao 4-1 na Bundes FC.

Hillary Shirao akituzwa baada ya kuibuka mfungaji bora. PICHA/ JOHN KIMWERE

Baada ya ufanisi huo mlezi huyo alisema ”Gogo Boys inaendelea kupiga hatua wala sina shaka kutaja kuwa wapo wachezaji wanaokuja kwa kasi ambao ndani ya muda mchache ujao endapo watazidi kutesa walivyo sasa watanasa dili za kushiriki soka la kulipwa nchini ama ugenini.

Bosi huyo aliwataka wanasoka wanaoibukia akiwamo Khubeib Asena na Abdulatiff ‘Dandi’ Ramadhan wazidi kukaza buti ili kufikia kiwango cha mwenzao mshambuliaji matata wa klabu hiyo Hillary Shirao.

Kwenye mashindano hayo fowadi huyo kwa mara ya pili mfululizo aliibuka mfungaji bora kwa kucheka na nyavu mara nane. Naye Bruce Omwena wa Ping FC alituzwa kama mlinda lango bora kwa kusaidia klabu yake kutofungwa mabao mengine licha ya kumaliza nafasi ya pili.

Viongozi wa klabu hiyo wanatoa wito kwa serikali iweke mikakati mwafaka ili kusaidia talanta za wachezaji chipukizi mashinani.

”Imegunduliwa kwamba taifa hili limefurika wachezaji wazuri kote nchini hasa wale hushiriki soka la viwango vya chini,” Chisira alisema na kuongeza kuwa makocha wa timu za taifa hawana budi kuwa wakitembea mashinani kusaka wachezaji wanaokuja ili kuwatambua na kuwaita katika vikosi vya taifa.

You can share this post!

Harambee Stars kupimana nguvu dhidi ya Sudan Kusini na...

Pigo kwa kipa Alisson Becker wa Liverpool baada ya baba...