• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Ghost Mulee asema anapata afueni baada ya ‘shughuli muhimu ya kimatibabu’ nchini India

Ghost Mulee asema anapata afueni baada ya ‘shughuli muhimu ya kimatibabu’ nchini India

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA wa timu ya taifa ya wanaume ya soka ya Kenya, Jacob Mulee anaendelea kupata nafuu nchini India alikolazwa.

Ghost, ambavyo kocha huyo anafahamika kwa jina la utani, alifichua Aprili 23, 2021, kuwa yuko hospitalini.

Alichapisha ujumbe kwenye mitandao yake ya kijamii ulioandamana na picha akiwa amevalia mavazi ya wagonjwa akipokea matibabu.

“Tunashukuru Mungu kuwa shughuli muhimu ya kimatibabu imekamilika salama. Nashughulikiwa vyema!” alisema kocha huyo mwenye umri wa miaka 52.

Haikubainika mara moja hali ya kiafya iliyofanya afike hospitalini, ingawa ripoti zinadai kuwa alichangia kaka yake figo. Kwa mujibu wa tovuti ya WhoOwnsKenya, Mulee, ambaye pia ni mtangazaji wa redioni, anatoka katika familia ya watoto 11. Yeye ni wa sita.

Inaonekana Mulee alielekea hospitalini siku chache tu baada ya mechi ya mwisho ya Harambee Stars ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) 2022 dhidi ya Togo kukamilika. Inasemekana amekuwa nchini humo kwa majuma matatu.

Stars ilibwaga Sparrow Hawks ya Togo 2-1 jijini Lome, ingawa ilikuwa tayari imeshabanduliwa kutoka Kundi G ambalo pia lilijumuisha Misri na Comoros zilifofuzu.

Baadhi ya Wakenya ambao wameelezea kumtakia nafuu ni pamoja na washambuliaji Michael “Engineer” Olunga (Al Duhail, Qatar), Ayub Timbe Masika (Vissel Kobe, Japan) na mwanamuziki Suzanna Owiyo. Hapa Taifa Leo pia sisi tunamtakia afueni ya haraka, yeye pamoja na nduguye.

You can share this post!

Ombi Oparanya, Joho waachie Raila urais 2022

Korti yakubali kesi ya Jowie, Maribe kusikilizwa hadharani