• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Giroud asaidia Chelsea kuzamisha Atletico Madrid kwenye mkondo wa kwanza wa UEFA

Giroud asaidia Chelsea kuzamisha Atletico Madrid kwenye mkondo wa kwanza wa UEFA

Na MASHIRIKA

BAO la dakika ya 68 kutoka kwa fowadi wa zamani wa Arsenal, Olivier Giroud, 34, liliwapa Chelsea ushindi wa 1-0 dhidi ya Atletico Madrid ya Uhispania katika mkondo wa kwanza hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumanne usiku.

Mechi hiyo ilichezewa mjini Bucharest, Romania kutokana na ukali wa masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Ushindi huo wa Chelsea uliendeleza rekodi ya kutopigwa kwa kikosi hicho katika jumla ya mechi nane zilizopita chini ya kocha mpya Thomas Tuchel aliyeaminiwa kuwa mrithi wa Frank Lampard mnamo Januari 2021.

Ni matokeo ambayo sasa yanawaweka Chelsea pazuri zaidi kufuzu kwa robo-fainali za UEFA. Chini ya kocha Diego Simeone, Atletico walijibwaga uwanjani kwa minajili ya mechi hiyo wakipigiwa upatu wa kuzamisha chombo cha Chelsea kwa wepesi. Hata hivyo, kipa Eduoard Mendy alifanya kazi ya ziada na kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na washambuliaji Luis Suarez na Joao Felix.

Giroud ambaye ni raia wa Ufaransa, aliagana rasmi na Arsenal mnamo Januari 2018 na kutua uwanjani Stamford Bridge kwa kima cha Sh2.5 bilioni pekee. Bao alilofunga dhidi ya Atletico lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na fowadi wa timu ya taifa ya Uingereza, Callum Hudson-Odoi na Timo Werner aliyejiunga na Chelsea mwanzoni mwa msimu huu kutoka RB Leipzig ya Ujerumani.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Nafasi ipo kuimarisha BBI iwafae Wakenya – Mudavadi

Raila achangamkia kupitishwa kwa BBI