• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Hatuna mpango wa kuuza Origi – Liverpool

Hatuna mpango wa kuuza Origi – Liverpool

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa Uingereza, Liverpool hawana mpango wa kuuza Mbelgiji mwenye asili ya Kenya, Divock Origi katika kipindi kifupi cha uhamisho kitakachofunguliwa Januari 2, 2021.

Divock, ambaye babaye Mike Okoth alikuwa mshambuliaji hodari wa klabu za Shabana na Tusker na timu ya taifa ya Harambee Stars kabla ya kuelekea Ubelgiji mnamo Julai 1992, amekuwa akihusishwa sana na uhamisho kwa majuma kadhaa.

Tetesi zimekuwa zikisema kuwa Origi anamezewa mate na Wolverhampton Wanderers inayoshiriki Ligi Kuu nchini Uingereza na miamba wa Italia Inter Milan.

Origi alijiunga na Liverpool mnamo Julai 29, 2014, wiki mbili baada ya kuwa mchezaji wa kwanza mwenye asili ya Kenya kufunga bao kwenye Kombe la Dunia alipozamisha Urusi 1-0 katika mechi ya mwisho ya makundi ya Ubelgiji nchini Brazil na pia kuwa mfungaji mwenye umri mdogo kwenye dimba hilo akiwa na umri wa miaka 19 na miezi miwili.

Msimu 2020-2021, Origi amepachika bao moja katika michuano minane ya Liverpool na kuchezeshwa dakika saba pekee kwenye Ligi Kuu baada ya kupoteza nafasi yake.

Kwa mujibu wa tovuti ya Liverpool Echo, “the Reds” hawatawasilisha Origi sokoni katika kipindi hiki, lakini waajiri hao wake wanasema hawatamzuia kuhama ofa nzuri ikitokea.

Origi, ambaye ni binamu ya kipa mkongwe Arnold Origi, alichezeshwa dakika moja ya mwisho Liverpool ikitoka 1-1 dhidi ya West Bromwich Albion mnamo Desemba 27.

Kocha Jurgen Klopp alimweka kitini mechi nzima timu hiyo ilipoumiza nyasi bure katika sare ya 0-0 dhidi ya Newcastle United mnamo Desemba 30.

Mshambuliaji huyo ametikisa nyavu mara 35 na kumega pasi 13 zilizozalisha mabao katika mechi 148. Kandarasi yake uwanjani Anfield imeratibiwa kukatika Juni 30, 2024.

  • Tags

You can share this post!

Corona: Kanisa latishia kususia chanjo

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Dhana na dhima ya malipo na ada...