• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 10:50 AM
Huyu Fofana “The Rock” apigiwa mahesabu na Man-United

Huyu Fofana “The Rock” apigiwa mahesabu na Man-United

Na GEOFFREY ANENE

WESLEY Fofana ni mmoja wa makinda wanaoongoza katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa kuchezeshwa sana na klabu zao, kutokana na utendakazi wao mzuri.

Mfaransa huyo anayechezea Leicester City yuko nyuma ya Bukayo Saka (Arsenal) na Ethan Ampadu (Sheffield United), kwenye orodha ya wachezaji walio chini ya umri wa miaka 21 ambao wamesakata boli dakika nyingi zaidi ligini msimu huu.

“Wes” ama “The Rock” jinsi Fofana anavyofahamika kwa majina ya utani, amechezeshwa na kocha Brendan Rodgers dakika 2,064 katika mechi 25 ligini. Saka na Ampadu wamesakata dakika 2,324 (mechi 28) na 2,091 (mechi 25) mtawalia.

Fofana ni beki wa kati. Alijiunga na mabingwa hao wa Uingereza msimu 2015-2016 kwa bei ya Sh4.7 bilioni kutokea Saint-Etienne mnamo Oktoba 2 mwaka jana.

Kandarasi yake itakatika Juni 30, 2025. “Akiwa na umri wa miaka 20 pekee, yeye ni mchezaji mwenye kipaji. Kila mechi ni hatua katika safari ya ukuaji wake ili kuhitimu kuwa beki stadi,” kocha Rodgers alinukuliwa Aprili akimsifu Fofana.

Mchezaji huyo mwenye asili ya Ivory Coast na pia Mali, alizaliwa mjini Marseille nchini Ufaransa mnamo Desemba 17, 2000. Anatoka katika familia ya watoto sita.Anasherehekea siku moja ya kuzaliwa na Martin Odegaard, 22, wa Arsenal pamoja na Andre Ayew, 31 wa Swansea.Fofana alianza uanasoka akiwa na umri wa miaka sita.

Alipitia mikononi mwa akademia za Repos Vitrolles (2006-2008), Bassin Minier (2008-2010), Pennes Mirabeau (2010-2011) na Bel Air (2011-2015) alikopiga hatua kubwa.

“Nilitumiwa mwanzoni na Bel Air kama mshambuliaji. Nililinganishwa sana na Didier Drogba kwa sababu ya kucheza katika safu ya mashambulizi na pia asili ya familia yangu ya Ivory Coast,” alinukuliwa akieleza historia yake.

Fofana alikuwa na matumaini makubwa ya kupiga hatua nzuri kwenye soka yake alipoingia Saint-Etienne mwaka 2015.Hii ni klabu ambayo imetoa nyota wengi wakiwemo Kurt Zouma (Chelsea), Allan Saint-Maximin (Newcastle) na Bafetimbi Gomes (Al Hilal Riyadh) pamoja na kocha wa timu ya taifa ya Georgia, Willy Sagnol.

Isitoshe, alipata mfano mzuri wa kuigwa kutoka kwa mvamizi matata wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang, aliyechezea Saint-Etienne kati ya 2011 na 2013.

Fofana aliimarika kwa haraka katika uchezaji wake akiingia timu ya Saint-Etienne ya wachezaji wasiozidi miaka 19, na kusaini kandarasi yake ya kwanza Mei 2018.Muda si muda aliingia timu ya pili (B) mwaka 2019, na kupanda hadi ile ya kwanza mwaka uo huo.

Alichezea Saint-Etienne jumla ya michuano 20 ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) kabla kulazimisha klabu hiyo imuuze kwa Leicester kwa ada ambayo ni ya pili ghali zaidi ugani King Power.

Mbelgiji Youri Tielemans ndiye sajili ghali kambini humo; aliingia Leicester kwa Sh5.7 bilioni akitokea Monaco.Fofana alikuwa pia akimezewa mate na West Ham, Monaco, Red Bull Salzburg, AC Milan, Arsenal, Everton na RB Leipzig aliposajiliwa na mabingwa hao wa zamani wa EPL kwa kima cha Sh4.7 bilioni.

Saint-Etienne ilikuwa imekataa ofa mbili za kwanza za Leicester za Sh3.2 bilioni na Sh3.6 bilioni.Katika mpango wa Fofana kuhamia Leicester, klabu hizo pia zilielewana kwamba Saint-Etienne itapokea asilimia 10 ya faida iwapo atauziwa klabu nyingine.

Tetesi zinasema kuwa miamba Manchester United wanatamani sana kumnyakua Fofana.Tovuti ya Spotrac inasema kuwa Fofana anapokea mshahara wa Sh148 milioni kila mwaka – Sh2.8 milioni kila wiki – kambini mwa Leicester.

Baadhi ya nguvu za mchezaji huyo ni weledi wake katika kuiba pasi za wapinzani, kusuka pasi na kushinda vita vya mipira ya juu.Kimataifa, difenda huyu amevalia jezi ya timu ya taifa ya Ufaransa ya wachezaji wasiozidi miaka 21, mara tatu.

Alikuwa katika timu ya Ufaransa iliyopepeta Liechtenstein 5-0 na Slovakia 1-0 mwaka 2020, na kulemewa na Denmark 1-0 Machi 2021 katika mechi za makundi za kufuzu kwa Kombe la Bara Ulaya la Under-21.

Inasemekana Leicester, almaarufu The Foxes, watakubali tu ahame King Power iwapo watapokea kitita cha Sh12.6 bilioni walizopata walipouzia Man-United difenda Harry Maguire mwaka 2019.

Maguire ndiye beki ghali zaidi duniani, baada ya kumpiku Virgil Van Dijk wa Liverpool aliyetua Anfield kwa bei ya Sh11.1 bilioni akitokea Southampton mnamo Januari 2018.

You can share this post!

KONDOO WA RUTO MATAANI

Tetesi kuhusu ukosefu wa sodo shuleni ni uongo mtupu –...