• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Julius Yego ajiuzulu kama nahodha wa timu ya taifa ya riadha ya Olimpiki

Julius Yego ajiuzulu kama nahodha wa timu ya taifa ya riadha ya Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA wa zamani wa dunia wa kurusha mkuki Julius Yego amejiuzulu kuwa nahodha wa timu ya riadha itakayoshiriki michezo ya Olimpiki mnamo Julai 23 hadi Agosti 8 mjini Tokyo, Japan.

Siku moja baada ya meneja mkuu wa timu ya Kenya ya Olimpiki Barnaba Korir kumkosoa vikali kwa kujifanya mwanaharakati asiyefahamu kweli wakati Yego kutetea mtimkaji wa mbio za mita 1,500 Kamar Etyang anayekodolea macho kutemwa kikosini, mshikilizi huyo wa rekodi ya Afrika alitangaza kujiuzulu kupitia mitandao ya kijamii.

“Mashabiki wangu nachukua fursa hii kusema nitawasikitisha kwa kuwa nimeamua kuachilia unahodha wa timu ya riadha inayoenda Olimpiki za Tokyo. Mazingira ya kuongoza timu hiyo kama nahodha siyo mazuri,” alitanguliza.

Aliongeza, “Poleni kwa kuwa sitaweza kuendelea kuwatumikia katika wadhifa huo, ingawa nilichaguliwa kufanya hivyo. Najua wanafahamu kwa nini nimechukua hatua hii. Nitasalia kuwa mmoja wa timu hii na nitasaidia popote nitahitajika. Tutachagua nahodha mpya hivi karibuni. Kabla ya kufanya hivyo, Eunice Sum ndiye atatuongoza. Kila la kheri sote Tokyo,” alisema jana.

Itakumbukwa Yego pia aligonga vichwa vya habari kabla ya sakata ya Olimpiki za Rio 2016 alipofika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi akielekea Brazil na kupata hakuwa amekatiwa tiketi. Kujiuzulu kwake hapo jana ni ishara kuwa mambo si mazuri katika kambi ya riadha ya timu inayoenda Olimpiki.

  • Tags

You can share this post!

Brazil yadengua Peru na kufuzu kwa fainali ya Copa America

Senegal yashinda Kundi B ya raga ya wachezaji 15 kila upande