• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Senegal yashinda Kundi B ya raga ya wachezaji 15 kila upande

Senegal yashinda Kundi B ya raga ya wachezaji 15 kila upande

Na GEOFFREY ANENE

SENEGAL imekamilisha Kundi B Raundi ya Pili ya Kombe la Afrika la raga ya wachezaji 15 kila upande kwa kunyamazisha Zambia 20-5 ugani Nyayo jijini Nairobi mnamo Julai 7.

Timu hiyo kutoka Magharibi mwa Afrika, ambayo iliduwaza wenyeji Kenya Simbas 20-19 mnamo Julai 3 uwanjani humo, imeshinda kundi hilo na kufuzu kushiriki Raundi ya Tatu mwaka 2022 ambayo mshindi wake ataingia Kombe la Dunia 2023 litakalofanyika nchini Ufaransa.

Mshindi kati ya Simbas na Zambia hapo Julai 11 pia atafuzu kushiriki Kombe la Afrika 2022 litakalojumuisha mataifa manane. Kenya watajibwaga uwanjani Nyayo wakihitaji ushindi pekee ili kujihakikishia tiketi hiyo.

Simbas ilirarua Copper Eagles ya Zambia 45-23 mjini Kitwe zilipokutana mara ya mwisho mwaka 2019 katika Kombe la Victoria Cup Senegal inaongoza Kundi B kwa alama nane ikifuatiwa na Kenya (moja) na Zambia (sifuri).  Kundi A linajumuisha Namibia, Ivory Coast na Madagascar. Linachezewa nchini Ivory Coast.

Wenyeji Ivory Coast walishangaza Namibia 24-13 Julai 3. Namibia na Madagascar wameratibiwa kukabiliana baadaye Julai 7. Kund C linakutanisha Uganda, Algeria na Ghana, huku Tunisia, Zimbabwe na Burkina Faso zikiunda Kundi D. Timu mbili za kwanza kutoka makundi hayo manne zitaingia Raundi ya Pili.

  • Tags

You can share this post!

Julius Yego ajiuzulu kama nahodha wa timu ya taifa ya...

KRU imani tele mashabiki wa raga watarejea viwanjani Desemba