• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
KCB FC ya Ligi Kuu ya FKF-PL yatema wachezaji watano

KCB FC ya Ligi Kuu ya FKF-PL yatema wachezaji watano

NA JOHN KIMWERE

TIMU ya KCB FC imetema wachezaji watano kwenye mikakati ya kujipanga upya tayari kushiriki kampeni za Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF-PL) muhula ujao.

Watano tayari wameelezwa kuwa hawapo kwenye mpango wa kocha Zedekiah ‘Zico’ Otieno kwenye mechi za msimu ujao.

Kocha huyo amewaonyesha watano hao mlango ili kutoa nafasi kwa wachezaji wapya kwenye jitihada za kujipanga kupigania taji hilo baada ya kulipoteza kwenye kampeni za msimu wa 2020/2021.

Orodha ya wachana nyavu hao inajumuisha nahodha wa zamani wa AFC Leopards, Robinson Kamura aliyejiunga na KCB kabla ya mwanzo wa muhula uliopita.

Alipojiunga na kikosi alikuwa anapata nafasi ya kucheza lakini kuelekea msimu kukamilika alikuwa mwenyeji wa benchi na kutoa nafasi kwa Nashon Alembi na kiungo Brian Ochieng.

Mwingine ni mnyakaji wa muda mrefu, David Okello aliyekuwa mlinda lango namba wani aliyejiunga na kikosi hicho kabla ya mwanzo wa kipute cha muhula uliyopita.

Mchezaji huyo aliyewahi kuchezea Mathare United, Tusker, Sofapaka na Thika United sasa itabidi asake makao mapya.

Mchezaji wa muda mrefu katika kikosi hicho nahodha, Simon Abuko aliyejiunga nacho akitokea AFC Leopards pia ameonyeshwa mlango.

Wengine wakiwa winga wa zamani wa Nzoia Sugar, Victor Omondi na Dennis Odhiambo aliyechezea timu hiyo tangia mwaka 2019.

Mchana nyavu huyo ametemwa licha ya kuwa amekuwa akipata nafasi ya kikosi cha kwanza.

Kadhalika Baraka Badi amevunja ndoa yake na kikosi hicho na kusajiliwa na timu ya Maafande wa Kenya Police.

  • Tags

You can share this post!

Mikopo: Wenye bodaboda walia

WANDERI KAMAU: Rais aturejesha enzi za giza kutwaa ardhi ya...

T L