• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 2:29 PM
Kocha Ronald Koeman kuendelea kudhibiti mikoba ya Barcelona

Kocha Ronald Koeman kuendelea kudhibiti mikoba ya Barcelona

Na MASHIRIKA

RONALD Koeman ataendelea kuwa kocha wa kikosi cha Barcelona kinachoshiriki Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Haya ni kwa mujibu wa rais wa kikosi hicho, Joan Laporta, ambaye amesema kwamba ameshiriki “mazungumzo yenye uwazi na ukweli” na mkufunzi huyo raia wa Uholanzi.

Koeman angali na mwaka mmoja kwenye mkataba wake na Barcelona japo vyombo vingi vya habari nchini Uhispania vimekuwa vikidai kwamba angetimuliwa na nafasi yake kutwaliwa na mchezaji wa zamani wa kikosi hicho, Xavier Hernandez.

Kulingana na Laporta, Barcelona wameteua kujishughulisha sokoni kwa kusajili wanasoka watakaofaulisha mipango yao ya kujisuka upya badala ya kutafuta kocha mpya.

Tayari Jordi Cruyff ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mchezaji matata wa Barcelona, Johan, ameteuliwa kuwa sehemu ya benchi ya kiufundi ya kikosi hicho ugani Camp Nou.

Cruyff, 47, alichezea Barcelona kati ya 1994 na 1996 na ataagana na kikosi cha Shenzhen FC anachokinoa kwa sasa katika Ligi Kuu ya China ili kutwaa majukumu mapya atakayopokezwa na Barcelona ugani Camp Nou.

Barcelona wamesema kwamba ujio wa Cruyff mnamo Agosti 1, 2021 ni sehemu ya mikakati mipya inayolenga kufanikisha maazimio ya kujisuka upya kwa miamba hao wa soka ya Uhispania chini ya Laporta.

Kwa mujibu wa gazeti a Football Daily nchini Uhispania, wanasoka wazoefu wa Barcelona hawapendi mbinu za ukufunzi wa Koeman na hawana imani naye kwa sababu hana ushawishi, mamlaka wala usemi wowote kikosini.

Katika kampeni za msimu huu wa 2020-21, Koeman, 58, aliongoza Barcelona kutwaa taji la Copa del Rey na kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) katika nafasi ya tatu nyuma ya Real Madrid na mabingwa Atletico.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa mabingwa hao mara 26 wa La Liga kukamilisha kampeni za kivumbi hicho nje ya mduara wa mbili-bora tangu 2007-08.

“Tumetathmini kwa kina matokeo ya Barcelona chini ya Koeman mnamo 2020-21. Tumekuwa na mazungumzo ya kina na Koeman na tumebadilisha msimamo wa baadhi ya wasimamizi wa kikosi waliotaka kocha apigwe kalamu,” akatanguliza.

“Maamuzi hayo ndiyo bora zaidi kwa Barcelona kwa sasa. Tuna furaha kutangaza kwamba Koeman atasalia nasi na ataendelea kudhibiti mikoba ya kikosi hiki,” akasema Laporta.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Uhasama wa kisiasa wa Sang na Cherargei wazuka tena mbele...

Nakuru kuwa jiji endapo Rais ataidhinisha uamuzi wa maseneta