• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Uhasama wa kisiasa wa Sang na Cherargei wazuka tena mbele ya kamati ya seneti

Uhasama wa kisiasa wa Sang na Cherargei wazuka tena mbele ya kamati ya seneti

Na CHARLES WASONGA

MALUMBANO makali yalizuka Alhamisi kati ya Gavana wa Nandi Stephen Sang’ na seneta wa kaunti hiyo Samson Cherargei kufuatia madai kuwa serikali ya kaunti hiyo ilitumia Sh1.39 bilioni kutekeleza miradi ghushi.

Kulingana na ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Nancy Gathungu serikali ya kaunti ya Nandi ilikamilisha mradi kati ya miradi 410 iliyoratibiwa kutekelezwa katika mwaka wa kifedh wa 2018/2019.

“Kutotekelezwa kwa miradi kulihujumu utekelezaji wa Mpango wa Maendelo wa Kaunti ya Nandi na Ruwaza ya Maendeleo ya 2030 nchini,” ilisema ripoti hiyo iliyokuwa ikikaguliwa jana na Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu (CPAIC).

Akirejelea ripoti hiyo Seneta Cherargei ambaye ni mwanachama wa kamati hiyo alidai kuwa kutotekelezwa kwa miradi iliyoratibiwa kwenye mpango wa maendeleo katika kaunti ya Nandi ni njia mojawapo “ambapo magavana hutumia kuiba pesa za umma.”

“Bw mwenyekiti ni mojawapo ya njia wanatumia magavana kuiba pesa za umma. Iweje kwamba wakaguzi wa hesabu waliweza kuthibitisha utekeleza wa mradi mmoja pekee kati ya 410 ilhali Sh1.39 bilioni zilitengewa mpango huo?” akauliza Bw Cherargei.

Kauli hiyo ilimkasirisha Gavana Sang’ ambaye alidai seneta huyo alitoa madai hayo kutokana na chuki na nia ya kumharibia sifa ili kumwangusha kisaisa.

“Ni haki kwa Seneta wangu kutoa madai ya uwongo mbele ya kamati kama hii. Bw Mwenyekiti mbona unamruhusu mwenzenu kuniharibia jina kwa kuniita mwizi ilhali hana mamlaka ya kuthibitisha madai hayo. Kamati kama hii haifai kugeuzwa kuwa jukwaa la kuendeleza siasa za kuchafuliana majina,” Bw Sang’ akamwambia mwenyekiti wa CPAIC Ochilo Ayacko, huku akionekana mwenye hasira.

Hapo ndio Bw Ayacko ambaye ni Seneta wa Rongo aliingilia kati na kutuliza hali kwa kuaamuru kwamba maafisa wa Bi Gathungu walirejee nyanjani katika kaunti ya Nandi na wathibitishe “hali ya miradi hiyo wakati huu.”

“Naagiza kwamba wakaguzi hao watakaporejea Nandi kuthibitisha hali ya miradi hiyo, waandamane na Seneta Cherargei ili naye aweze kujionea. Kisha wakaguzi waandae ripoti maalum na kuwasilisha kwa kamati hii,”

“Ripoti hiyo ndio itatupa mwelekeo kuhusu iwapo miradi hiyo ilitekelezwa hao la. Kando na hayo madai yanayotolewa hapa yatasalia tu siasa za Nandi ambazo hazituhusu,” akasema Bw Ayacko.

Kauli hiyo iliungwa mkono na maseneta Christopher Langat (Bomet), Johnnes Mwaruma (Taita Taveta) na Njeru Ndwiga (Embu).

You can share this post!

Duale aitaka serikali ya Korane iimarishe huduma Garissa

Kocha Ronald Koeman kuendelea kudhibiti mikoba ya Barcelona