• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Kocha Ronald Koeman kunoa tena timu ya taifa ya Uholanzi baada ya fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar

Kocha Ronald Koeman kunoa tena timu ya taifa ya Uholanzi baada ya fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar

Na MASHIRIKA

KOCHA Ronald Koeman atakuwa mkufunzi wa timu ya taifa ya Uholanzi kwa mara ya pili baada ya kukamilika kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Koeman, 59, atajaza nafasi ya Louis van Gaal, 70, ambaye alifichua kwamba anaugua saratani ya kibofu mnamo Aprili 3, 2022.

“Ni fahari kubwa kuwatangazia kwamba nitarejea kudhibiti tena mikoba ya Uholanzi baada ya kukamilika kwa fainali za Kombe la Dunia. Natazamia sana fursa hiyo ili nikabiliane na changamoto mpya na kadri ninavyolenga kuongoza kikosi kujivunia mafanikio tele,” akasema Koeman.

Koeman ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Southampton na Everton nchini Uingereza, aliwahi kuwatia makali masogora wa timu ya taifa ya Uholanzi kati ya 2018 na 2020.

Katika awamu yake ya kwanza, Koeman ambaye alichezea Uholanzi mara 78 akiwa beki, aliaminiwa kujaza nafasi ya kocha Dick Advocaat mnamo Februari 2018 baada ya mkufunzi huyo kujiuzulu kwa kushindwa kusaidia kikosi chake kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka huo.

Chini ya Koeman, Uholanzi walitinga fainali ya Uefa Nations League mnamo 2019 ambapo walipokezwa na Ureno kichapo cha 1-0. Aidha, alisaidia Uholanzi kufuzu kwa fainali za Euro 2020 ambapo kikosi hicho kiliambulia nafasi ya pili nyuma ya Ujerumani kwenye hatua ya makundi ya kampeni za Euro 2020.

Koeman hakusimamia mechi yoyote iliyotandazwa na Uholanzi kwenye Euro 2020 kwa kuwa kipute hicho kiliahirishwa kwa mwaka mmoja zaidi na kikasakatwa kati ya Juni na Julai 2021 kwa sababu ya janga la corona. Wakati huo, Koeman alikuwa tayari ametua nchini Uhispania kudhibiti mikoba ya Barcelona katika Ligi Kuu ya La Liga mnamo Agosti 2020.

Akiwa Barcelona, Koeman aliongoza miamba hao kuzoa taji la Copa del Rey mnamo Aprili 2021. Hata hivyo, alishindwa kusaidia kikosi hicho kutwaa taji la La Liga na akatimuliwa mnamo Oktoba 2021.

Baada ya Van Gaal ambaye ni kocha wa zamani wa Manchester United kufichua hali yake ya ugonjwa, nahodha wa Uholanzi Virgil van Dijk alisema anataka “kucheza katika fainali zijazo za Kombe la Dunia kwa namna ambayo mkufunzi huyo hatawahi kusahau”.

Uholanzi ambao wamepoteza fainali ya Kombe la Dunia mara tatu, wametiwa katika Kundi A kwa pamoja na Ecuador, Senegal na wenyeji Qatar. Mchuano utakaowakutanisha na Senegal kwenye Kombe la Dunia utatandazwa mnamo Novemba 21 huku fainali ya kipute hicho ikiratibiwa kufanyika Disemba 18, 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mradi wa ufugaji nyuki wasaidia jamii kujikimu

Washtakiwa kushindwa kulipia mvinyo

T L