• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Koeman achemkia wanahabari kwa kuuliza mustakabali wake kitaaluma baada ya Barcelona kukabwa koo na Granada ligini

Koeman achemkia wanahabari kwa kuuliza mustakabali wake kitaaluma baada ya Barcelona kukabwa koo na Granada ligini

Na MASHIRIKA

KOCHA Ronaldo Koeman “hatajibu maswali yoyote kuhusu mustakabali wake kambini mwa Barcelona” baada ya bao la dakika ya mwisho kutoka kwa Ronald Araujo kuwavunia miamba hao wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) sare ya 1-1 dhidi ya Granada mnamo Jumatatu usiku.

Matokeo hayo duni yaliyosajiliwa na Barcelona katika uwanja wao wa nyumbani yanatarajiwa kumtia Koeman presha ya kunyanyua waajiri wake katika mechi zijazo au la apigwe kalamu.

Araujo ambaye kwa kawaida ni beki mkabaji, alikuwa akiwajibishwa na Barcelona kama fowadi na akafunga bao la kusawazisha mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya Coutinho Meneses Duarte kuweka Granada kifua mbele katika dakika ya pili.

Barcelona walipokezwa kichapo hicho siku tano baada ya kupepetwa na Bayern Munich kwenye mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Granada walijitosa ulingoni wakipania kusajili ushindi wao wa kwanza msimu huu na wa pili chini ya kipindi cha misimu miwili ugani Camp Nou.

“Tulibadilisha mtindo wetu wa kucheza. Ilitulazimu kutegemea wanasoka waliokuwa katika hali sawa ya kuwajibishwa na kikosi. Huwezi kucheza tiki-taka wakati ambapo huna wachezaji wa kufanikisha mtindo huo wa pasi fupi za haraka,” akatanguliza Koeman.

“Ilibidi tufanye jinsi tulivyofanya. Tulijaribu kushinda kwa kutumia njia mbadala. Hatukuwa na wachezaji wenye uwezo wa kupiga chenga au walio na kasi ya juu,” akaongeza kocha huyo raia wa Uholanzi.

Mbali na Araujo, mwanasoka mwingine wa Barcelona aliyejituma zaidi dhidi ya Granada ni Sergi Roberto japo makombora yake yalidhibitiwa vilivyo na Luis Maximiano.

Barcelona ambao hawajapoteza mchuano wowote wa La Liga kufikia sasa msimu huu, sasa wanashikilia nafasi ya saba jedwalini kwa alama nane kutokana na mechi nne. Granada wanakamata nafasi ya 17 kwa pointi tatu.

Barcelona watacheza dhidi ya Cadiz na Levante kabla ya kufunga safari ya kuelekea Ureno kupimana ubabe na Benfica katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ishara Chelsea na Liverpool hawatashikika katika EPL muhula...

Mlima Kenya ‘kuwatahini’ wawaniaji wa urais 2022