• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:44 AM
Ishara Chelsea na Liverpool hawatashikika katika EPL muhula huu

Ishara Chelsea na Liverpool hawatashikika katika EPL muhula huu

Na MASHIRIKA

JAPO ni mara tano pekee ambapo klabu zimetandaza mechi hadi kufikia sasa kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) muhula huu, dalili zote zinaashiria kwamba Chelsea ndio tishio kubwa zaidi kwa washindani wengine wakuu katika kipute hicho.

Chelsea wamekuwa wakiimarika tangu Januari makali yao yalipofufuliwa na kocha Thomas Tuchel ambaye kwa pamoja na Mjerumani mwenzake, Jurgen Klopp wa Liverpool, wanazidi kuwapa mashabiki ‘kitu’ cha kufuatilia katika gozi la EPL.

Hata bahati isiposimama na Chelsea jinsi ilivyokuwa dhidi ya Liverpool mwezi jana ambapo beki Reece James alionyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha kwanza, masogora wa Tuchel walisalia thabiti na kuondoka ugenini na alama moja muhimu.

Washikilizi hao wa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) waliendeleza ubabe wao Jumapili kwa kutandika Tottenham Hotspur 3-0 katika mechi iliyodhihirisha utajiri wa vipaji katika benchi ya Chelsea na ubora wa mbinu za mkufunzi Tuchel.

Kuletwa ugani kwa N’Golo Kante kujaza nafasi ya Mason Mount kuliwapa Chelsea nafasi kubwa ya kuwatamalaki Spurs katika safu ya kati huku Marcos Alonso akipata fursa ya kupanda hadi ndani ya kijisanduku cha wapinzani na kutoa krosi zilizotatiza mabeki wa Spurs.

Chelsea kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 13 sawa na Liverpool na Manchester United ambao pia wameshinda mechi nne kati ya tano za ufunguzi wa muhula huu. Vikosi hivyo vitatu ndivyo vya pekee ambavyo havijapoteza mechi yoyote ya EPL kufikia sasa muhula huu.

Brighton wanafunga mduara wa nne-bora kwa alama 12, mbili zaidi kuliko mabingwa watetezi Manchester City na Everton wanaotarajiwa kuagana rasmi na kiungo matata raia wa Colombia, James Rodriguez, anayemezewa na klabu moja nchini Qatar.

Ingawa ni mechi tano pekee ambazo zimepigwa katika EPL msimu huu, Chelsea tayari wamepepetana na Arsenal, Liverpool na Spurs na wakajizolea alama saba kutokana na mechi hizo ‘ngumu’ za ugenini. Hata walipopoteza alama mbili dhidi ya Liverpool kwa kuambulia sare ya 1-1, Chelsea walicheza kipindi chote cha pili wakiwa na wanasoka 10 pekee uwanjani. Hiyo ni ishara ya jinsi masogora wa Tuchel walivyo thabiti kiakili na imara katika safu ya ulinzi.

Kwa mujibu wa Alan Shearer ambaye ni mchanganuzi maarufu wa soka nchini Uingereza, kusajiliwa kwa mfumaji Romelu Lukaku ni ishara ya kiu ya Tuchel kutaka kutamalaki kivumbi cha EPL muhula huu hata ingawa waajiri wake walitwaa taji la UEFA msimu jana bila kujivunia maarifa ya Mbelgiji huyo ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Everton, Man-United na Inter Milan.

“Chelsea ndicho kikosi thabiti zaidi katika EPL kwa sasa. Wamejisuka ipasavyo na tutarajie soka ya kusisimua kutoka kwao muhula huu. Klabu hiyo inajivunia mseto mzuri wa chipukizi matata na wanasoka wazoefu wenye tajriba pevu japo Liverpool na Man-United pia wako imara,” akasema Shearer.

Chelsea walikamilisha kampeni za EPL msimu jana katika nafasi ya nne kwa alama 19 nyuma ya Man-City na ndicho kikosi cha pili baada ya Man-United (mechi 690) kuwahi kushinda michuano 600 katika historia ya kipute cha EPL.

Mtihani ujao kwa Chelsea ni gozi kali la EPL dhidi ya Man-City ugani Stamford Bridge wikendi hii. Hata hivyo, wanapigiwa upatu wa kutia kapuni alama tatu ikizingatiwa kwamba walikomoa miamba hao wa kocha Pep Guardiola mara tatu msimu jana, ikiwemo kwenye fainali ya UEFA.

Kufikia sasa, matokeo ya Chelsea na Liverpool ligini yanawiana katika kila mchuano. Chelsea walianza kampeni zao kwa kutandika Crystal Palace 3-0 kabla ya kupiga Arsenal 2-0 na kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Liverpool. Kabla ya kupepeta Spurs 3-0, walikuwa wamepokeza Aston Villa kichapo sawa na hicho.

Kwa upande wao, Liverpool walipepeta Norwich City 3-0 kabla ya kupiga Burnley 2-0. Baada ya kulazimishiwa na Chelsea sare ya 1-1, miamba hao waliwakomoa Leeds United na Palace 3-0 mtawalia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Odunga aokoa wanyonge

Koeman achemkia wanahabari kwa kuuliza mustakabali wake...