• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Lewandowski apokea tuzo ya haiba kubwa kutoka kwa Rais wa Poland

Lewandowski apokea tuzo ya haiba kubwa kutoka kwa Rais wa Poland

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Robert Lewandowski amepokezwa tuzo ya haiba kubwa ya Commander’s Cross of the Order of Polonia Restituta kutoka kwa Rais wa Poland, Andrzej Duda kutokana na ukubwa na upekee wa mchango wake katika ulingo wa soka akichezea Bayern Munich ya Ujerumani na timu ya taifa ya Poland.

Tuzo hiyo huwa maalumu kwa maafisa wa jeshi na raia wa kawaida wanaodhihirisha matendo bora ya kuipa jamii mwelekeo mwema nchini Poland.

Lewandowski, 32, ndiye mtu wa tatu baada ya aliyekuwa Rais wa Poland, Lech Walesa na Rais wa zamani wa Amerika, Dwight D. Eisenhower kuwahi kupokea tuzo hiyo.

Taji hilo linaongeza idadi ya mataji katika kabati la Lewandowski ambaye tayari amejivunia makombe mbalimbali chini ya kipindi cha msimu mmoja na nusu uliopita.

Lewandowski alituzwa mahsusi kutokana na mchango wake katika kampeni za msimu wa 2019-20 ambapo alitia kapuni mataji ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), DFB-Pokal (German Cup) na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Sogora huyo aliibuka mfungaji bora katika kila mojawapo ya mapambano hayo.

Isitoshe, Lewandowski aliongoza pia kikosi cha Bayern kutia kibindoni taji la German League Cup (DFL) na UEFA Super Cup huku akisaidia Poland kufuzu kwa fainali za Euro 2020 ambazo sasa zitatandazwa mwaka huu baada ya kuahirishwa kutokana na janga la corona.

Katika kiwango cha mtu binafsi, Lewandowski alituzwa Mchezaji Bora wa Mwaka kwa upande wa wanaume na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na shirika la Globe Soccer. Pia alitawazwa Mshambuliaji Bora wa Mwaka na UEFA na shirika la Tuttosport Golden.

Baada ya kutuzwa na Rais Duda, Lewandowski aliahidi kujituma zaidi katika mapambano yote mengineyo yaliyoko mbele yake huku akilenga kutwaa taji la Mfungaji Bora wa Bundesliga (Torjagerkanone) kwa mara nyingine msimu huu.

Kufikia sasa, Lewandowski amepachika wavuni mabao 35 katika Bundesliga na alifunga mawili katika ushindi wa 4-0 uliosajiliwa na Bayern dhidi ya VfB Stuttgart katika gozi la Bundesliga wikendi iliyopita.

Mabao hayo yalimwezesha kumpita Klaus Fischer na kuingia katika nafasi ya pili nyuma ya Gerd Muller kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote katika historia ya Bundesliga.

Lewandowski kwa sasa anahitaji magoli sita pekee kutokana na mechi 10 zijazo muhula huu ili kuvunja rekodi ya Muller aliyewahi kupachika wavuni jumla ya mabao 40 katika msimu mmoja wa Bundesliga.

Lewandowski na sogora Krzysztof Piatek wa Hertha Berlin watakuwa tegemeo kubwa la Poland kwenye mchuano ujao wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar watakapowaendea Uingereza uwanjani Wembley, London mnamo Machi 31, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mtahiniwa wa KCPE afa baada ya kujifungua, familia ya...

Kipa Sergio Romero kuagana rasmi na Man-United mwishoni mwa...