• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Ligi ya daraja la pili yapamba moto

Ligi ya daraja la pili yapamba moto

Na CHARLES ONGADI

MICHUANO ya Ligi ya Taifa Daraja la Pili kanda ya kaskazini zoni A iliendelea kushika kasi eneo la Pwani huku michuano kumi ikipigwa mwishoni mwa juma.

Katika mechi zilizogaragazwa Jumapili, Shanzu United FC iliikomoa Kishada goli 1-0 katika pambano la kusisimua katika uwanja wa Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Shanzu.

Hata hivyo, Shanzu United ililazimika kutumia kila mbinu kabla ya kupata bao hilo la pekee katika dakika ya 92 kupitia Heri Juma.

Kocha wa Shanzu United James Sewe akitoa ushauri kwa mfungaji wa bao la pekee Heri Juma katika pambano lao dhidi ya Kishada FC ugani Shanzu TTC. Picha/ Charles Ongadi

Katika mchuano huu ambao nusura utibuke baada ya kufungwa kwa bao hilo, wachezaji wawili, Adam Washe wa Shanzu United na Mohammed ‘ Kileso’ Juma walioneshwa kadi nyekundu na refa wa pambano hili Francis ‘ Mariga ‘ Musyoka baada ya kugeuza uwanja kuwa jukwaa la masumbwi.

Katika mechi yao ya siku ya jumamosi, Kishada ilipigana kufa na kupona kabla ya kuambulia matokeo ya sare ya 1-1 dhidi ya Progressive FC ya Malindi uwanjani Hassan Joho Girls, Kisauni.

Katika mchuano huu, Progressive ilitangulia kuona lango kupitia mfungaji wao bora Edysson Katana kwa njia ya penelti kabla ya Kishada kusawazisha kupita Simon Wanjiru kwa njia ya kichwa.

Nayo Tikki FC ya Taita Taveta ilirudi nyumbani kwao mikono mitupu baada ya kuzimwa na Green Marine kwa mabao 2-0 siku ya jumamosi na kuongezwa mabao kama yayo hayo siku ya jumapili na Nacet FC katika michuano iliyogaragazwa huko Kwale.

Ziwani Youth FC nayo iliona cha mtema kuni katika ziara yao eneo la Magarini baada ya kuzimwa 2-1 na wenyeji Beach Bay FC, Jumamosi.

Bahari Youth ambayo imekuwa ikijikokota katika michuano yake , iliambulia sare dhidi ya wageni wao Borrussia Dortmund ya Takaungu katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Mtwapa, Kilifi, Jumapili.

Sparki Youth ikaandikisha matokeo ya sare 1-1 dhidi ya Super Matuga uwanjani Tudor Primary huku Mariakani FC ikiitandika Yanga FC ya Malindi kwa mabao 2-1 uwanjani Mariakani Village Polytechnic, Jumapili.

Maji Bombers FC ikaikwaruza Kilifi All Stars mabao 2-1 katika pambano la kusisimua iliyochezwa Lango Baya, Malindi.

Michuano hii inatarajiwa kupamba moto mwishoni mwa wiki hii katika viwanja mbalimbali eneo la Pwani.

  • Tags

You can share this post!

Aliyekuwa afisa wa mechi ya UEFA iliyotibuka kati ya PSG na...

Cavani kujiunga na Boca Juniors ya Argentina baada ya...