• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 12:11 PM
Liverpool wapepeta Villarreal katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya UEFA

Liverpool wapepeta Villarreal katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya UEFA

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL walipiga hatua kubwa katika juhudi za kutinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara nyingine baada ya kutandika Villarreal 2-0 katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali mnamo Jumatano usiku ugani Anfield.

Ushindi huo uliweka hai matumaini ya Liverpool kutia kapuni jumla ya mataji manne kwenye kampeni za msimu huu. Zaidi ya kufukuzia taji la UEFA, Liverpool tayari wametawazwa mabingwa wa Carabao Cup na wanawania pia Kombe la FA na ufalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Baada ya kipindi cha kwanza kukamilika kwa sare tasa, Liverpool walijiweka uongozini kunako dakika ya 53 baada ya kombora la nahodha na kiungo Jordan Henderson kumbabatiza beki Pervis Estupinan na kumwacha hoi kipa wa Villarreal, Geronimo Rulli.

Sadio Mane alifunga bao la pili la Liverpool katika dakika ya 55 baada ya kuandaliwa krosi safi na Mohamed Salah.

Mchuano wa mkondo wa pili utapigiwa nchini Uhispania mnamo Mei 3, 2022 na mshindi baada ya mikondo yote miwili atakutana ama na Manchester City au Real Madrid kwenye fainali itakayochezewa jijini Paris, Ufaransa mnamo Mei 28, 2022.

Villarreal walishuka dimbani wakipigiwa upatu wa kukomoa Liverpool baada ya kudengua Juventus na Bayern Munich katika hatua za 16-bora na robo-fainali mtawalia.

Chini ya kocha Unai Emery ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Sevilla, Paris Saint-Germain (PSG) na Arsenal, Villarreal waliibana sana ngome yao katika kipindi cha kwanza huku Liverpool wakipoteza nafasi chache walizopata.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ujenzi wa barabara kurejelewa baada ya mashambulio kukoma

AU, UN zaunga jeshi la EAC kukabili waasi DRC

T L