• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
Lukaku kuongoza mashambulizi ya Ubelgiji dhidi ya Wales

Lukaku kuongoza mashambulizi ya Ubelgiji dhidi ya Wales

Na MASHIRIKA

FOWADI Romelu Lukaku ameungana sasa na wanasoka wenzake katika timu ya taifa ya Ubelgiji baada ya vipimo vya afya kubainisha kwamba hana virusi vya corona.

Wiki jana, visa vinne vya maambukizi ya corona viliripotiwa kambini mwa Inter Milan ambao ni waajiri wa Lukaku. Kati ya wanasoka wanne waliougua Covid-19 katika kikosi hicho ni kipa Samir Handanovic.

Tukio hilo lilisababisha kuahirishwa kwa mchuano wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) uliokuwa ukutanishe Inter Milan ya kocha Antonio Conte na Sassuolo uwanjani San Siro, Italia.

Awali, usimamizi wa Inter Milan ambao kwa sasa wanadhibiti kilele cha jedwali la Serie A kwa alama 65, walikuwa wamepanga kuzuia wanasoka wao kuondoka Italia na kurejea katika nchi zao kwa mapambano yajayo ya kimataifa.

Ubelgiji wamepangwa kuanza kampeni zao za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar mnamo Machi 24, 2021 kwa gozi dhidi ya Wales.

Baadaye, watapepetana na Jamhuri ya Czech jijini Prague mnamo Jumamosi ya Machi 27 kabla ya kualika Belarus jijini Brussels mnamo Machi 30, 2021.

Chini ya kocha Roberto Martinez, Ubelgiji watakosa huduma za viungo Eden Hazard na Axel Witsel wanaochezea Real Madrid na Borussia Dortmund mtawalia. Wawili hao wanauguza majeraha ya miguu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

VISABABISHI: Tatizo la damu kuganda mwilini si jambo geni...

Uhuru asifu Pombe kwa kuhepa ukopaji