• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mabeki Maguire na Tierney kurejea katika vikosi vyao vya kwanza wakati wa mechi ya Euro kati ya Uingereza na Scotland

Mabeki Maguire na Tierney kurejea katika vikosi vyao vya kwanza wakati wa mechi ya Euro kati ya Uingereza na Scotland

Na MASHIRIKA

KOCHA Gareth Southgate amethibitisha kwamba beki Harry Maguire, 28, amepona jeraha na atakuwa katika hali shwari ya kuwajibishwa katika mchuano ujao wa Kundi D dhidi ya Scotland kwenye fainali za Euro mnamo Juni 18, 2021.

Mechi hiyo itampa pia kocha Steve Clarke wa Scotland jukwaa la kumkaribisha kikosini beki Kieran Tierney wa Arsenal. Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24 alikosa gozi la ufunguzi kati ya Scotland na Jamhuri ya Czech mnamo Juni 14 kwa sababu ya jeraha la mguu. Jamhuri ya Czech ilisajili ushindi wa 2-0 kwenye mechi hiyo.

Maguire ambaye ni nahodha wa Manchester United, amekuwa nje akiuguza jeraha la kifundo cha mguu kwa zaidi ya mwezi mmoja uliopita.

Tyrone Mings alijaza pengo la Maguire kambini mwa Uingereza katika mechi iliyowakutanisha na Croatia mnamo Juni 13. Alishirikiana vilivyo na John Stones na wakasaidia kikosi chao kusajili ushindi wa 1-0.

“Amesema anajihisi vizuri na yuko tayari kwa kibarua kilichopo mbele. Amekuwa akishiriki mazoezi kwa kujituma sana na matazamio yake ni kuunga kikosi cha kwanza katika mechi ijayo dhidi ya Scotland,” akasema Southgate.

Maguire ambaye ni beki wa zamani wa Hull na Leicester City, alipata jeraha mwishoni mwa kipindi cha pili wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyokutanisha waajiri wake Manchester United na Aston Villa mnamo Mei 9, 2021.

Jeraha hilo lilimnyima pia fursa ya kuwajibikia Man-United dhidi ya Villarreal kwenye fainali ya Europa League na michuano miwili ya kirafiki iliyosakatwa na Uingereza kirafiki dhidi ya Austria na Romania.

Licha ya kuuguza jeraha, Maguire bado alijumuishwa na Southagate kwenye kikosi chake cha wanasoka 26 kwa ajili ya fainali za Euro zilizoahirishwa mnamo 2020 kwa sababu ya janga la corona.

Uingereza wanapigiwa upatu wa kuibuka kileleni mwa Kundi D linalojumuisha pia Jamhuri ya Czech, Croatia na Scotland. Ufanisi huo utawakutanisha na kikosi kitakachoambulia nafasi ya pili katika Kundi F linalojumuisha Hungary, Ujerumani, Ufaransa na Ureno ambao ni mabingwa watetezi wa Euro.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

‘Hakuna kifo cha corona jana Jumatano’

Kocha Benitez pazuri zaidi kuwa mrithi wa Ancelotti kambini...