• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 10:50 AM
Macho kwa Ruth Chepng’etich watimkaji 400 wakishiriki mbio za nyika za kitaifa

Macho kwa Ruth Chepng’etich watimkaji 400 wakishiriki mbio za nyika za kitaifa

Na GEOFFREY ANENE

ZAIDI ya wakimbiaji 400 akiwemo malkia wa marathon Ruth Chepng’etich, wataonyeshana ubabe kwenye mbio za nyika za kitaifa katika Chuo cha Mafunzo ya Magereza mjini Ruiru, kaunti ya Kiambu, leo Jumamosi, Januari 21.

Chepng’etich kutoka Idara ya Magereza atawania taji la kitengo cha kilomita 10 kilichovutia zaidi ya washiriki 90.

Baadhi ya wapinzani wake wakuu ni bingwa wa dunia mbio za mita 3,000 za chipukizi Teresia Gateri, mshindi wa nyika Pwani Irene Mkungo, nambari sita kwenye michezo ya Afrika 5000m Lydia Jeruto, bingwa wa kaunti ya Nairobi Evangeline Makena na mshindi wa medali ya fedha ya 3,000m ya Riadha za Dunia za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, Zenah Jemutai.

Vita vikali pia vitashuhudiwa katika mbio za wanaume za 10km zitakazoleta pamoja zaidi ya washiriki 100.

Baadhi ya majina makubwa hapa ni bingwa wa zamani wa Olimpiki na dunia 1500m Asbel Kiprop pamoja na Leonard Bett, Alfred Barkach, Abel Mutai, Panuel Mkungo na Reuben Longosiwa.

Mkimbizi Francois Msafiri (DR Congo), Gert Brienne “Rubani Mkimbiaji” (Uholanzi) na Herman Selle (Tanzania), Samuel Kibet (Uganda) ni baadhi ya watimkaji wakigeni wanaoshiriki.

Bingwa wa Afrika mbio za 800 Jarinter Mawia, mshikilizi wa rekodi ya dunia 3,000m kuruka viunzi na maji Beatrice Chepkoech na bingwa wa zamani wa Olimpiki 1,500m Timothy Cheruiyot watakuwa vivutio katika kitengo cha mbio mseto za kupokezana vijiti.

Timu 17 zitashiriki. Majina mengi makubwa hayashiriki kwa sababu wako kambini kwa mbio za nyika za dunia zitakazoandaliwa Februari 18 nchini Australia.

  • Tags

You can share this post!

Mung’aro afika kortini kujitetea asipoteze kiti

Riggy G akutana na wabunge wa Jubilee kutoka Mlima Kenya...

T L