• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 3:57 PM
Madereva tayari kupaisha mashine zao kuwania alama kwenye duru ya tatu ya mashindano ya KCB Autocross

Madereva tayari kupaisha mashine zao kuwania alama kwenye duru ya tatu ya mashindano ya KCB Autocross

Na GEOFFREY ANENE

MBIVU na mbichi kuhusu madereva hodari katika mashindano ya mbio za Autocross itajulikana katika duru ya tatu mjini Eldoret hapo Jumamosi.

Shughuli ya kukagua magari yatakayoshiriki ilifanywa na kukamilika Ijumaa. Madereva watashiriki michujo minne huku mitatu yenye kasi nzuri ikitumiwa kuamua watakaoshiriki fainali.

Baadhi ya madereva nyota wanaotarajiwa kupaisha mashine zao ni pamoja na Lovejyot Singh (4WD Turbo), Yuvraj Rajput (Bambino), Azaad Manji (2WD Turbo) na Kiana Rajput (Pee Wee). Mpinzani mkuu wa karibu wa Lovejyot, Eric Bengi hashiriki duru ya Eldoret ambayo timu ya Decko Racing inatumai kuwa mojawapo ya familia chache kufagia mataji kwenye mashindano hayo ya siku moja.

Katika mashindano hayo yatakayofanyika katika eneo la Harton Grange na kudhaminiwa na benki ya KCB, timu ya Decko itaingiza madereva wanne wakiwemo mabingwa watetezi Yuvraj Rajput katika kitengo cha Bambino, Kirit Rajput (Open Class) na Wayne Fernandes (Quad).

Kirit, ambaye anaongoza timu hiyo ya madereva wanne, atakuwa akifukuzia ushindi wake wa pili msimu huu.

Dereva msichana Kiana Rajput ndiye pekee hana taji katika mashindano haya.

Mwaka 2019, Kiana alihitimu umri wa kupata alama wa miaka saba katikati ya msimu kwa hivyo hakuweza kutimiza sharti la kushiriki asilimia 75 ya mashindano.

Wayne Fernandes amejawa na matumaini siku ya mashindano inapokaribia.

“Ni mara yangu ya kwanza kushiriki mashindano ya Autocross mjini Eldoret. Barabara mpya za sehemu hii ambayo raundi hii ya tatu ya Autocross itafanyika pia ni mtaani mwangu kwa hivyo nasubiri familia na marafiki kujitokeza kutushangilia na kutupa motisha,” alisema Wayne.

  • Tags

You can share this post!

Corona: DP Ruto asitisha mikutano yake ya hadhara

Waandishi wa Thika wapewa hamasisho kuhusu wajibu wao