• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 6:50 AM
Manchester United mwishowe wakubali kumsajili Jadon Sancho kwa Sh12 bilioni

Manchester United mwishowe wakubali kumsajili Jadon Sancho kwa Sh12 bilioni

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United hatimaye wameafikiana na Borussia Dortmund kuhusu uhamisho wa kiungo mvamizi raia wa Uingereza, Jadon Sancho ambaye kwa sasa atatua uwanjani Old Trafford kwa Sh12 bilioni.

Ofa hiyo ndiyo ya tatu kwa Man-United kutoa kwa ajili ya Sancho, 21, baada ya ofa za awali za Sh9.4 bilioni na Sh11.3 bilioni kukataliwa na Dortmund.

Maafikiano kati ya vikosi hivyo viwili ni zao la mazungumzo ya kina yaliyohusisha mwenyekiti wa Dortmund, Hans-Joachim Watzke na naibu mwenyekiti wa Man-United, Ed Woodward.

Kwa mujibu wa maagano hayo, Sancho anatarajiwa sasa kutia saini mkataba wa miaka mitano utakaomshuhudia akitia mfukoni mshahara wa Sh54.6 milioni kwa wiki uwanjani Old Trafford.

Mshahara huo utakuwa mara tatu zaidi kuliko ule ambao kwa sasa anapokezwa kambini mwa Dortmund. Donyell Malen ambaye ni raia wa Uholanzi anayechezea sasa kikosi cha PSV Eindhoven anatarajiwa kuwa kizibo cha Sancho kambini mwa Dortmund.

Huku Sancho akiwa bado sehemu ya kikosi kinachowakilisha Uingereza kwenye kampeni zinazoendelea za Euro, Malen anatarajiwa kutua Ujerumani kufikia mwisho wa wiki hii na kurasimisha uhamisho wake kambini mwa Dortmund.

Hii ni baada ya Jamhuri ya Czech kubandua Uholanzi kwenye hatua ya 16-bora ya Euro.

Sancho amefungia Dortmund mabao 50 kutokana na mechi 137 na amepachikia Uingereza magoli matatu kutokana na mechi 20.

Katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita, sogora huyo wa zamani wa Manchester City amehusika katika mabao 109 ambayo yamefungwa na Dortmund na alicheka na nyavu mara mbili waliposhinda RB Leipzig kwenye fainali ya German Cup mnamo Mei 2021.

Man-United walikosa kujinasia maarifa ya Sancho miezi 12 iliyopita baada ya Dortmund kuwawekea bei ya Sh16.8 bilioni. Sancho alijiunga na Dortmund mnamo Agosti 2017 baada ya kuagana na Man-City kwa Sh1.5 bilioni.

Sasa atakuwa mchezaji wa pili ghali zaidi kuwahi kutua Old Trafford baada ya kiungo Paul Pogba kusajiliwa na Man-United kwa kima cha Sh12.4 bilioni kutoka Juventus ya Italia mnamo 2016.

Kuondoka kwa Sancho pia ni pigo kwa Man-City ikizingatiwa kwamba Dortmund sasa hawatakuwa radhi kumwachilia pia fowadi wao matata raia wa Norway, Erling Haaland aondoke uwanjani Signal Iduna Park muhula huu.

Man-City ambao wanatafuta mfumaji mrithi wa Sergio Aguero aliyeyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Barcelona baada ya mkataba wake ugani Etihad kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mkenya Mathew Sawe aingia Olimpiki mchezo wa High Jump

Liverpool na Man-United katika vita vya kuwania maarifa ya...