• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 7:55 PM
Liverpool na Man-United katika vita vya kuwania maarifa ya fowadi Kingsley Coman wa Bayern Munich

Liverpool na Man-United katika vita vya kuwania maarifa ya fowadi Kingsley Coman wa Bayern Munich

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL wamesema wamepiga hatua kubwa katika juhudi za kumsajili fowadi wa Bayern Munich, Kingsley Coman, ambaye pia anahemewa na Manchester United.

Liverpool ya kocha Jurgen Klopp inawania maarifa ya Coman, 25, ili awe kizibo cha Divock Origi anatazamiwa kuondoka uwanjani Anfield muhula huu.

Mkataba wa sasa kati ya Coman na Bayern unatarajiwa kukatika mwishoni mwa msimu wa 2021-22 na waajiri wake wana hofu ya kumwachilia atafute hifadhi mpya kwingineko bila ada yoyote muhula ujao.

Kwa mujibu wa gazeti la Sport1 nchini Ujerumani, Liverpool wako radhi kuweka mezani kima cha Sh6.7 bilioni ili kujinasia huduma za Coman aliyefungia Bayern bao la pekee na la ushindi katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) iliyowakutanisha na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa katika msimu wa 2019-20 jijini Lisbon, Ureno.

Coman amewajibishwa na timu ya taifa ya Ufaransa mara 31. Amekuwa akihudumu kambini mwa Bayern nchini Ujerumani tangu 2015 ila akatumwa Juventus kwa mkopo kabla ya kurejea uwanjani Allianz Arena mnamo 2017.

Mbali na Origi, mwanasoka mwingine anayetarajiwa kubanduka kambini mwa Liverpool muhula huu ni kiungo raia wa Uswisi, Xherdan Shaqiri. Kiungo matata raia wa Uholanzi, Georginio Wijnaldum, tayari ameondoka Liverpool na kuyoyomea Ufaransa kujiunga na Paris Saint-Germain (PSG).

Ujio wa Coman unatarajiwa kuzidisha viwango vya ushindani katika safu ya mbele ya Liverpool inayojivunia maarifa ya Mohamed Salah, Sadio Mane, Roberto Firmino na Diogo Jota.

Liverpool tayari wamejinasia huduma za beki Ibrahima Konate aliyeagana na RB Leipzig ya Ujerumani kwa kima cha Sh5.4 bilioni.

Chini ya Klopp, Liverpool walikamilisha kampeni za EPL mnamo 2020-21 katika nafasi ya nne nyuma ya Chelsea, Manchester United na Manchester City waliotawazwa mabingwa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Manchester United mwishowe wakubali kumsajili Jadon Sancho...

Jinsi unavyoweza kujua una ukosefu wa protini mwilini