• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Marseille wamfuta kazi kocha Villas-Boas na kumwajiri Jorge Sampaoli

Marseille wamfuta kazi kocha Villas-Boas na kumwajiri Jorge Sampaoli

Na MASHIRIKA

KIKOSI cha Olympique Marseille kimetamatisha rasmi mkataba wa kocha Andre Villas-Boas aliyesimamishwa kazi kwa muda mnamo Februari 2, 2021 baada ya kukosa sera na falsafa za waajiri wake.

Nafasi ya Villas-Boas ambaye pia amewahi kunoa Tottenham Hotspur, Chelsea na Zenit Saint Petersburg, imetwaliwa na kocha wa zamani wa timu za taifa za Arnetina na Chile, Jorge Sampaoli, 60.

Sampaoli ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Sevilla nchini Uhispania, alipokezwa mkataba wa miaka miwili utakaotamatika rasmi mnamo 2023 kambini na Marseille.

Villas-Boas ambaye ni raia wa Ureno, hakuridhishwa na hatua ya Marseille inayoshiriki Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) kumsajili kiungo Olivier Ntcham kutoka Celtic katika siku ya mwisho ya muhula uliopita wa usajili mnamo Januari 2021.

Marseille ambao ni mabingwa mara 10 wa taji la Ligue 1, walitamatisha kandarasi ya Villas-Boas baada ya kuhudumu kambini mwao kwa kipindi cha miezi 19. Kikosi hicho kilitwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya mwisho mnamo 1993.

Villas-Boas alipokezwa mikoba ya Marseille mnamo 2019 na akawaongoza kutinga nafasi ya pili nyuma ya PSG kwenye kampeni za Ligue 1 katika msimu uliopita wa 2019-20.

Hadi wakati ambapo Villas-Boas alisimamishwa kazi kambini mwa Marseille, kikosi hicho kilikuwa kikishikilia nafasi ya tisa kwenye msimamo wa jedwali la Ligue 1 na kilikuwa tayari kimebanduliwa kwenye hatua ya makundi ya kampeni za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Tangu Mreno huyo atemwe kwenye benchi ya kiufundi, kocha Nasser Larguet aliyepokezwa nafasi ya kushikilia mikoba ya kikosi aliongoza waajiri wake katika mechi saba na wakapoteza moja pekee. Mchuano huo ni ule ulioshuhudia Marseille wakipokezwa kichapo cha 2-0 na mabingwa watetezi wa Ligue 1, PSG.

Sampaoli tayari amewasili nchini Ufaransa kutoka Brazil kuanza kazi kambini mwa Marseille baada ya kukamilisha kipindi cha siku saba za karantini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ronaldo aweka rekodi ya ufungaji wa mabao Ulaya

Raila awaonya Wapwani dhidi ya kuunda chama