• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mashindano ya kuogelea sasa kuanza Ijumaa jijini Mombasa

Mashindano ya kuogelea sasa kuanza Ijumaa jijini Mombasa

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

MASHINDANO ya kuogelea ambayo yalisimamishwa sababu ya janga la corona, yanatarajiwa kuanza kufanyika eneo la Pwani kuanzia siku ya Ijumaa.

Wapiga mbizi wa eneo la Pwani wanatarajia kupigania ushindi wakati wa mashindano ya CASA Age-Group Swimming Championship kufanyika mjini Mombasa Ijumaa hadi Jumapili ya wiki hii.

Chama cha Kuogelea cha Pwani (CASA) kimetangaza kinasubiri uthibitisho wa mwisho juu ya kufunguliwa kwa mashindano ya kuogelea ili watoe mwelekeo zaidi juu ya mashindano hayo ikiwemo sehemu yatakapofanyika.

Katibu wa Chama cha Kuogelea cha Pwani (CASA) Larissa Hart amesema programu ya jinsi mashindano hayo yatakavyofanyika na tahadhari zitakazotakiwa kufanyika zitafahamishwa kwa maofisa wa klabu za wapiga mbizi ambao watakuwa wa umri kuanzia miaka 10 na zaidi.

Larissa amesema kuna umuhimu kwa wapiga mbizi wa sehemu hiyo kushiriki kwenye mashindano ili waweze kuimarisha nyakati zao kwa kupigania kuchaguliwa kwenye timu za taifa zitakazoshiriki kwenye mashindano mbalimbali.

“Ninawaomba wahusika wa klabu mbalimbali mujitayarishe kwa mashindano haya na kuna umuhimu wa kusambaza habari hizi kwa kila timu na kuwahimiza waogeleaji kufuata kanuni zinazohitajika za kujikinga na usambazaji wa Covid-19,” akasema.

Eneo la Pwani ndilo pekee lilotoa waogeleaji wawili ambao watashiriki kwenye Michezo ya Olimpiki yanayofanyika huko Tokyo nchini Japan.

Wapiga mbizi hao ni Daniel Rosafio wa Bandari SC na Emily Muteti wa Mombasa Aquatics.

Shirikisho la Kuogelea la Kenya (KSF) limewachagua Fakhry Mansoor wa Bandari Swimming Club kuwa kocha mkuu wa waogeleaji hao huko Japan hali Abdulmalik Abubakar wa Mombasa Aquatics akiwa meneja wao.

You can share this post!

Mashabiki wapokea kikosi cha Italia kwa shangwe na mbwembwe...

Kampeni ya kugawa Huduma Namba yaanza