• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mbio za Ras Al Khaimah zafutwa

Mbio za Ras Al Khaimah zafutwa

Na GEOFFREY ANENE

SIKU mbili baada ya kufunga zoezi la kujiandikisha kushiriki mbio za kilomita 21 za Ras Al Khaimah za mwaka 2021 nchini Milki za Kiarabu, waandalizi wametangaza kuzifutilia mbali kutokana na hofu za kiusalama wakati huu janga la virusi vya corona.

Mastaa 60 kutoka mataifa mbalimbali wakiwemo Wakenya Geoffrey Kamworor, Hellen Obiri, Kibiwott Kandie, Peres Jepchirchir, Eric Kiptanui na Brigid Kosgei walikuwa wamethibitisha kutimka mbio hizo katika kisiwa cha Al Marjan mnamo Februari 19.

Kandie na Jepchirchir ni washikilizi wa rekodi za dunia za mbio za kilomita 21 za wanaume na wanawake za dakika 57:32 na 65:16 mtawalia. Naye Kosgei ni mwanamke mwenye kasi ya juu kabisa katika mbio za kilomita 42 za mseto ya saa 2:14:04. Kandie alishinda Ras Al Khaimah Half Marathon 2020.

Kamworor, ambaye alirejea ulingoni Juma lililopita baada ya kuwa nje kwa muda mrefu akiuguza majeraha aliyopata alipogongwa na pikipiki, alikuwa amepanga Ras Al Khaimah Half Marathon kuwa mbio zake za kwanza za kilomita 21 tangu ajali.

Obiri naye alitaka mbio za Ras Al Khaimah Half Marathon ziwe zake za kwanza kabisa ndefu baada ya kung’ara katika zile za uwanjani za mita 5,000 na mita 10,000.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya mbio hizo za kifahari Jumatano, waandalizi walisema walichukua uamuzi huo baada ya kutathmini hali kwa kina.

“Tumepima hali tukaona ni busara kuahirisha makala ya 15 ya mbio za Ras Al Khaimah Half Marathon kutoka Februari 19, 2021 Hadi mwaka 2022. Tumechukua hatua hii muhimu ili kulinda maslahi ya washiriki, mashabiki na wafanyakazi kutokana na hali inayobadilikabadilika.”

“Usalama wa wageni wote wanaozuru mji wa Ras Al Khaimah unasalia muhimu kabisa na tunawashukuru kwa kuelewa. Tunatumai washiriki wote waliokuwa wamepanga kuja katika mji huu kuufurahia watafika katika fukwe zetu kutalii na kujionea tamaduni zetu hapa Milki za Kiarabu,” taarifa hizo zilisema huku waandalizi wakiahidi kurejeshea washiriki wote fedha zao walizotumia kama kiingilio cha mashindano.

  • Tags

You can share this post!

Sonko aangua kilio kortini, adai kuna jaribio la kumuua

Sonko hatarini kushtakiwa kwa madai ya ugaidi