• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Miaka yangu mitano kambini mwa Man-City sasa inaleta mantiki na maana zaidi – Pep Guardiola

Miaka yangu mitano kambini mwa Man-City sasa inaleta mantiki na maana zaidi – Pep Guardiola

Na MASHIRIKA

KOCHA Pep Guardiola wa Manchester City amesema kwamba kuongoza kikosi hicho kuingia fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mara ya kwanza katika historia sasa ni “jambo lenye mantiki na maana zaidi” katika kipindi cha miaka mitano ya kuhudumu kwake uwanjani Etihad.

Mabao mawili kutoka kwa kiungo mvamizi Riyad Mahrez yalisaidia Man-City kudengua Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa kwa jumla ya magoli 4-1 kwenye hatua ya nusu-fainali.

Japo Man-City wanahitaji sare au ushindi katika mechi moja kati ya nne zilizosalia kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu na kutia kapuni taji la tatu la kipute hicho chini ya Guardiola, kocha huyo alikuwa ameshindwa kuongoza waajiri wake zaidi ya hatua ya robo-fainali kwenye UEFA.

“Hii ni hatua kubwa ambayo imepigwa na Man-City. Kuingia fainali ya UEFA sasa inatuaminisha kwamba tumefanya kazi kubwa katika kipindi cha miaka minne au mitano iliyopita,” akasema mkufunzi huyo raia wa Uhispania.

Chini ya Guardiola, Man-City walibanduliwa kwenye robo-fainali za UEFA katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita dhidi ya Olympique Lyon, Tottenham Hotspur na Liverpool. Aidha, walipoteza mechi za mikondo miwili za hatua ya 16-bora dhidi ya AS Monaco mnamo 2016-17 ambao ulikuwa msimu wa kwanza wa Guardiola ugani Etihad.

Huu ni msimu wa 10 mfululizo kwa Man-City kunogesha soka ya UEFA na walikuwa awali wametinga nusu-fainali mara moja ambapo walipigwa 1-0 na Real Madrid kwenye mikondo miwili mnamo 2015-16 wakiwa chini ya kocha raia wa Chile, Manuel Pellegrini.

Tangu umiliki wa Man-City utwaliwe na bwanyenye Sheikh Mansour mnamo 2008, miamba hao wametia kibindoni mataji manne ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), mawili ya Kombe la FA na sita ya League Cup.

Sasa wana fursa nzuri zaidi ya kunyanyua ufalme wa UEFA huku wakitarajiwa kukutana na mshindi wa nusu-fainali ya pili kati ya Chelsea ya Uingereza na Real Madrid ya Uhispania.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kutokuwepo kwa Mbappe si kisingizio cha PSG kupigwa na...

Suluhu asaidia kusuluhisha matatizo kati ya Wakenya na...