• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Mikakati na mipango yangu kambini mwa Arsenal itaanza kuzaa matunda hivi karibuni – Arteta

Mikakati na mipango yangu kambini mwa Arsenal itaanza kuzaa matunda hivi karibuni – Arteta

Na MASHIRIKA

KOCHA Mikel Arteta amesema mipango na mikakati yake ya muda mrefu kambini mwa Arsenal itaanza kuzaa matunda ya kuridhisha hivi karibuni baada ya kila kitu kuwekwa sawa ugani Emirates.

Arsenal kwa sasa wanashikilia nafasi ya 10 kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na tayari wamebanduliwa kwenye gozi la Kombe la FA walilokuwa wakilitetea muhula huu. Miamba hao wa zamani wa soka ya Uingereza walidenguliwa na Southampton kwenye Kombe la FA mnamo Januari 2021.

Huku matumaini ya kuwa miongoni mwa vikosi vitakavyokamilisha kampeni za EPL msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora yakionekana kudidimia zaidi, fursa ya pekee kwa Arsenal kunogesha soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao ni kutwaa taji la Europa League muhula huu.

“Nimekuwa nikifanyia kazi mradi fulani unaolenga kuwapa Arsenal uthabiti wa kipindi kirefu kijacho. Ni mradi ambao baadhi ya mashabiki wameanza kuona matokeo yake katika kila mchuano ila matunda mazuri zaidi yataanza kuvunwa hivi karibuni,” akatanguliza kocha huyo raia wa Uhispania aliyewahi pia kuchezea Everton na Arsenal.

“Lengo langu ni kuunda kikosi kilicho thabiti na chenye uwezo wa kuhimili ushindani mkali ligini. Nataka timu itakayofahamu umuhimu wa kushinda mechi dhidi ya mpinzani yeyote na kuweka mbele matamanio ya mashabiki pamoja na matarajio ya maafisa wa benchi ya kiufundi,” akaendelea Arteta.

“Ilivyo, dalili zote zinaashiria kwamba tunaelekea huko japo panda-shuka fulani za hapa na pale ndani na nje ya uwanja zimechangia kuwepo kwetu katika nafasi tunayoishikilia kwa sasa jedwalini,” akaongeza kwa kusisitiza kwamba njia ya pekee ya kumwaminisha mashabiki kwamba kuna mradi muhimu anaoushughulikia kikosini ni kwa wanasoka wake kuanza kushinda kila mechi.

Arteta anahisi kwamba angalikuwa amefanya usajili muhimu zaidi kambini mwa Arsenal iwapo hazina yao ya fedha haingelemezwa na janga la corona ambalo liliwasababishia hasara ya Sh6.7 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2019-20.

Arsenal hawajawahi kucheza mechi mbele ya maelefu ya mashabiki wao uwanjani Emirates kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita kwa sababu ya corona. Hata hivyo, mashabiki 2,000 pekee waliojikalia katika sehemu mbalimbali za uwanja waliruhusiwa kuhudhuria baadhi ya michuano mnamo Disemba 2020 baada ya wadau kulegeza baadhi ya kanuni za kudhibiti msambao wa Covid-19.

Kwa mujibu wa Arteta, asichokijua kufikia sasa ni iwapo hasara iliyokadiriwa na Arsenal itaathiri pakubwa uwezo wa kikosi wa kujishughulisha katika soko la uhamisho wa wachezaji mwishoni mwa msimu huu kwa kuwa lengo lake ni kujinasia maarifa ya wanasoka kadhaa wa haiba kubwa zaidi katika takriban kila idara uwanjani.

“Itatulazimu kusajili wanasoka zaidi wenye uwezo wa kututambisha ipasavyo katika soka ya Uingereza na hata bara Ulaya. Tumetambua yaliko matatizo yetu na mradi nilio nao umelenga kuziba mapengo hayo yaliyopo kabla ya kikosi kianze kuangusha miamba wa soka nchini Uingereza na bara Ulaya na kutwaa mataji,” akaongeza Arteta.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Diwani ataka uvunaji mchanga uruhusiwe Makuyu kuepusha...

Dkt Mwangangi awahakikishia wabunge chanjo ya Covid-19 ni...