• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
Mkenya Brian Mandela asherehekea kushinda Ligi Kuu ya Afrika Kusini na klabu yake ya Mamelodi Sundowns

Mkenya Brian Mandela asherehekea kushinda Ligi Kuu ya Afrika Kusini na klabu yake ya Mamelodi Sundowns

Na GEOFFREY ANENE

MAMELODI Sundowns anayochezea Mkenya Brian “Mandela” Onyango imetawazwa rasmi kuwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini kwa mara nne mfululizo na 11 kwa jumla mnamo Jumamosi.

Sundowns imezamisha wageni wao Cape Town City 3-0 katika mechi ya kufunga msimu kupitia bao la Lyle Lakay lililopatikana dakika ya 10 na mawili katika kipindi cha pili kutoka kwa Mnamibia Peter Shalulile.

Beki Onyango, ambaye msimu huu alijipata akiwa mnyakaji wakati Mganda Denis Onyango aliumia kidole katika dakika za lala-salama dhidi ya Supersport United mnamo Mei 26, aliingia katika nafasi ya Mosa Lebusa dakika ya 30. Ni mara ya kwanza kabisa Mandela ameshinda taji hilo.

Sundowns imekamilisha msimu kwa alama 67 kutokana na michuano 30 kwenye ligi hiyo ya klabu 16. Ilifuzu kushiriki Klabu Bingwa Afrika pamoja na nambari mbili AmaZulu (alama 54) nayo nambari tatu Orlando Pirates (alama 50) itashiriki Kombe la Mashirikisho la Afrika.

Kaizer Chiefs anayochezea kiungo Mkenya Anthony Akumu imekamilisha katika nafasi ya nane kwa alama 36. Imezaba TS Galaxy 1-0 uwanjani Mbombela katika mechi ambayo Akumu alikuwa kitini.

Chiefs ingali katika Klabu Bingwa Afrika msimu huu baada ya kumaliza Ligi Kuu ya 2019-2020 katika nafasi ya pili. Italimana na Wydad kutoka Morocco ugenini mnamo Juni 19 na kualika timu hiyo Juni 26 katika mechi za nusu-fainali.

  • Tags

You can share this post!

Mke na mwanawe Matasi kufanyiwa upasuaji Jumatatu

Hydroponic: Mfumo bora wa kilimo kukwepa kero ya magonjwa