• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 8:50 AM
Moraa ni miongoni mwa 7 waliopokea tuzo ya heshima kutoka kwa Rais Ruto

Moraa ni miongoni mwa 7 waliopokea tuzo ya heshima kutoka kwa Rais Ruto

Na AYUMBA AYODI

BINGWA wa michezo ya Jumuiya ya Madola mbio za mita 800, Mary Moraa yuko katika orodha ya wanamichezo saba waliopokea tuzo ya heshima kutoka kwa Rais William Ruto katika sherehe za siku ya Jamhuri.

Mbali na Moraa, ambaye alitwaa nishani ya shaba kwenye Riadha za Dunia jimboni Oregon, Amerika mwezi Julai, mshindi wa medali ya shaba ya mbio mseto za kupokezana vijiti Hellen Syombua na mshikilizi wa zamani wa rekodi ya kitaifa ya mbio za mita 100 Thomas Musinde, pia walituzwa.

Moraa, Syombua na Musinde walipokea tuzo ya Heshima ya Head of State Commendation (HSC).

Moraa na Syombua ni makonstebo wa polisi naye Musinde ni sajini katika majeshi ya KDF. Maafisa wengine kutoka vikosi vya usalama waliopokea tuzo hizo ni walengaji shabaha wa kutumia bunduki Thomas Kamitu, Abdulahi Nur na Inspekta wa Polisi Cornelius Koros.

Walengaji hao wa shabaha wamewakilisha Kenya kimataifa ikiwemo katika mashindano ya Imperial Bisley nchini Uingereza.

Rais wa Shirikisho la Tenisi ya mezani Kenya (KTTA) Andrew Mudibo pia alipokea tuzo hiyo katika kitengo cha raia.

Moraa alishinda taji la Jumuiya ya Madola mwezi Agosti kabla ya kubeba ubingwa wa riadha za Diamond League mjini Zurich, Uswisi.

Moraa alifuta rekodi ya kitaifa ya mbio za mita 400 mara mbili mwaka huu, akitimka umbali huo kwa sekunde 50.84 wakati wa mashindano ya kuchagua timu ya taifa ya Riadha za Dunia mwezi Juni na kuiimarisha hadi 50.67 mjini Brussels, Ubelgiji mwezi Septemba. Syombua alishikilia rekodi ya 400m ya sekunde 51.09 kabla ya Moraa kuifuta.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

Wanasiasa waonywa wasiingilie mchakato wa kuajiri walimu...

Tennis Kenya kuadhimisha miaka 100 kwa kuombea Okutoyi...

T L