• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Mpango wa Willian kujiunga na Inter Miami watibuka baada ya kiungo huyo wa Arsenal kudai mshahara mkubwa ajabu

Mpango wa Willian kujiunga na Inter Miami watibuka baada ya kiungo huyo wa Arsenal kudai mshahara mkubwa ajabu

Na MASHIRIKA

INTER Miami wamekatiza mchakato wa kumsajili kiungo wa Arsenal na timu ya taifa ya Brazil, Willian Borges, 32.

Kwa mujibu wa gazeti la SunSport, kutibuka kwa mpango huo kumechangiwa na hatua ya Willian kudai mshahara mkubwa wa hadi Sh1.4 bilioni kwa mwaka ambao ni takriban Sh26 milioni kwa wiki.

Tukio hilo ni pigo kwa kocha Phil Neville aliyekuwa na matarajio ya kumtema Rodolfo Pizarro wa Mexico na kumfanya Willian kuwa kizibo chake kwenye Major League Soccer (MLS).

Kufikia sasa, aliyekuwa fowadi matata wa Juventus na timu ya taifa ya Argentina, Gonzalo Higuain, ndiye sogora anayedumishwa kwa mshahara mkubwa zaidi kambini mwa Inter Miami. Nyota huyo ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Chelsea, Napoli, AC Milan na Real Madrid ndiye nahodha wa Inter Miami ambao wanampokeza ujira wa Sh653 milioni kwa mwaka, sawa na takriban Sh13 milioni kwa wiki.

Japo mkataba wa sasa kati ya Arsenal na Willian unatarajiwa kutamatika rasmi mnamo 2023, yamekuwa matamanio yake kuagana na kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta baada ya kutoridhisha katika kampeni za msimu wa 2020-21.

Beki wa zamani wa Arsenal na West Bromwich Albion, Kieran Gibbs, anatarajiwa kuingia katika sajili rasmi ya Inter Miami mnamo Julai 2, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Washukiwa wawili wa wizi wa mabavu wakamatwa jijini Nairobi

‘Wanajeshi 11 walioangamia kwenye ajali ya helikopta...