• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 9:55 AM
Mwamba kurejea nyumbani Nairobi Railway Club ujenzi wa kituo cha basi ukikamilika

Mwamba kurejea nyumbani Nairobi Railway Club ujenzi wa kituo cha basi ukikamilika

Na AYUMBA AYODI

KLABU ya raga ya Mwamba itarejea kutumia uwanja wake wa nyumbani wa Nairobi Railway Club.

Kwa mujibu wa afisa mmoja wa ngazi ya juu wa klabu hiyo, Shirika la Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) limekubalia klabu hiyo iendelee kutumia uwanja huo.

Shirika hilo lilishauri klabu hiyo kutohama kabisa katika uwanja huo kwa sababu itakubaliwa kurejea mara tu ujenzi wa kituo cha basi utakamilika kwa sababu uwanja huo wa raga hautaguswa.

Afisa huyo alisema kuwa NMS pia ina habari nyingine nzuri kwa Mwamba kuwa itakarabati uwanja huo na sehemu ya mashabiki kuketi, bila ya klabu hiyo kugharamika.

“Wametuonyesha hata ramani ya kituo cha basi na uwanja wetu na nadhani ujenzi huo ukikamilika, tutakuwa na uwanja mzuri,” alisema afisa huyo ambaye hakutaka kutajwa.

“Viti vya mashabiki vitaongezwa. Utakuwa uwanja mzuri sana kwa sababu magari yatashusha abiria karibu na lango letu. NMS ilisema kuwa imechelewa katika ujenzi huo kwa hivyo itaharakisha kuukamilisha,” alieleza.

Mwamba imekuwa ikitafuta makao mapya baada ya kuambiwa iondoke katika uwanja huo mnamo Septemba 2020 ili kutoa fursa ya ujenzi wa kituo kipya cha basi na kupanuliwa kwa barabara kuu ya juujuu ya Nairobi (Expressway).

Mwamba, ambayo imekuwa ikifanyia mazoezi yake katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Nairobi unaotumiwa na klabu ya ligi ya daraja ya pili Mean Machine, ilitangaza Januari 2020 kuwa inatafuta uwanja mpya.

Rais wa klabu hiyo Alvas Onguru alisema kuwa wanalenga viwanja vitatu jijini Nairobi wanavyoweza kutumia, lakini akadokeza kuwa watahitaji miezi mitatu kujenga uwanja unaofaa.

Onguru, ambaye hakufichua maeneo hayo matatu, alikuwa amedokeza kuwa mmoja wa wamiliki wa maeneo hayo mawili alikuwa amekubali kuwakodisha kwa kipindi cha miaka 30 naye mwingine alitaka kodi ya kila mwezi.

Mwamba, ambayo ni mojawapo ya klabu kongwe nchini Kenya, ilipoteza uwanja wake ilipoamrishwa ihame kutoka Nairobi Railway Club ambao ilikuwa imetumia kwa miaka 42.

Mwamba ni mojawapo ya klabu nne ambazo hazikujiandikisha kushiriki Ligi Kuu (Kenya Cup) msimu 2021 ulioanza Jumamosi iliyopita.

Imetangaza kuwa itarejea mashindanoni na itakuwa uwanjani mnamo Machi 13 kupepetana na Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Mwamba imechangia mashujaa wa raga nchini wakiwemo Edward Rombo na ndugu Collins Injera na Humphrey Kayange.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

Fujo, hongo kwenye uchaguzi mdogo Nakuru

Chanjo ya corona hatarini