• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Chanjo ya corona hatarini

Chanjo ya corona hatarini

NA BENSON MATHEKA

MATUMAINI ya Wakenya kwamba kuwasili kwa chanjo za corona kutasaidia kukabili virusi hivyo yatabakia ndoto, iwapo wanasiasa, maafisa wa serikali na wafanyiashara walaghai wataamua kuendeleza mazoea yao ya kuvuruga miradi ya umma.

Hofu ambayo imezuka ni kuhusu uwezekano wa chanjo hizo kukosa kufikia wananchi wanaolengwa na badala yake kuibwa na watu wenye ushawishi serikalini.

Wasiwasi huu unatokana na historia ya wanasiasa, wafanyibiashara na maafisa wa serikali kuvuruga miradi mingi inayonuiwa kusaidia umma na hasa maskini.

Kulingana na Seneta wa Kaunti ya Narok, Ledama Ole Kina, wanasiasa wanafaa kujitenga na chanjo hiyo ili iweze kufaidi maskini kwanza.

“Maskini ndio wanaofaa kupata chanjo ya corona kwanza na sio waheshimiwa,” Bw Ole Kina alisema.

Kulingana na serikali, chanjo hiyo kwanza itapewa watu walio msitari wa mbele kukabili janga hilo wakiwemo wahudumu wa afya, maafisa wa usalama, walimu na watu walio katika hatari kuu ya kuambukizwa.

Lakini wanahofia kwamba wanasiasa na watu wengine wenye ushawishi watanyakua chanjo hiyo kujikinga wao binafsi na familia zao, na kuacha walio kwenye hatari hasa maskini wakiteseka.

Hali hii tayari imeshuhudiwa Lebanon ambako wabunge walikuwa wa kwanza kupewa chanjo kinyume na serikali ya nchi hiyo ilivyokuwa imeahidi kuwa watakaochanjwa kwanza ni wahudumu wa afya na walio kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa.

Mtindo huo pia umeshuhudiwa Peru, Ecuador, Ufilipino na Uhispania, na ikizingatiwa kiwango cha juu cha ufisadi hapa Kenya pamoja na ubinafsi wa viongozi, huenda chanjo hiyo ikaingia kwenye msururu wa sakata za kila mara nchini.

Wakati corona ilipozuka nchini na serikali ikatangaza mipango mingi ya kukabiliana nayo, wanasiasa walaghai wakishirikiana na wafanyibiashara na maafisa wa serikali walivuruga mipango hiyo kwa kuiba pesa zilizotengwa. Matokeo yalikuwa kuongezeka kwa maambukizi na vifo.

Kwenye sakata ya corona mwaka jana, wafanyibiashara na maafisa walaghai waliteka Mamlaka ya Kusambaza Dawa (KEMSA), ambapo kampuni za washirika wao zilipatiwa zabuni za zaidi ya Sh7.2 bilioni kuuza vifaa vya kujikinga dhidi ya corona kwa bei ya juu kupindukia.

Haya yalitendeka wakati madaktari walikuwa wakihatarisha maisha yao kupima na kushughulikia wagonjwa wa corona.

Maswali pia yameibuka kuhusu usalama wa chanjo hiyo ikizingatiwa kuwa wahudumu wa afya wamekuwa wakiiba dawa katika hospitali za umma na kuuzia hospitali na maduka ya kibinafsi, jambo ambalo linafanya maskini kulemewa na gharama ya maisha.

Kulingana na Wizara ya Afya, chupa za chanjo zitawekwa alama za kuzifuatilia kuhakikisha kwamba hazitaibwa.

Mkuu wa jopokazi la kushauri serikali kuhusu Covid 19, Dkt Willis Akhwale alisema kila chupa itakuwa na alama ya kuifuatilia inaposafirishwa na kuthibitisha ni mali ya serikali.

Hata hivyo, baadhi ya Wakenya wanasema hii haiwezi kuzuia maafisa wa serikali kuiba chanjo hiyo: “Ni dawa ngapi tunanunua katika maduka ya watu binafsi zilizo na chapa na nembo ya serikali?” Anahoji David Kahura, mkazi wa jiji la Nairobi.

Miradi mingine ambayo inawafanya Wakenya wengi kushuku hata chanjo ya Covic itageuka sakata ni mpango wa Kazi kwa Vijana ulionuiwa kusaidia vijana kupata ajira, ambao uligeuzwa mfereji wa kuiba mabilioni ya pesa za umma.

Zaidi ya Sh10 bilioni zilipotea kupitia sakata hiyo na kuacha vijana waliokuwa na matumaini ungewafaidi wakiteseka.

Pesa za mradi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, ambapo serikali ilipoteza zaidi ya Sh20 bilioni na bwawa la Chemususu, Kaunti ya Nakuru ambalo limekwama.

Mipango mingine ambayo ililenga kufaidi maskini lakini ikaingiliwa na wanasiasa ni ununuzi wa mahindi kutoka kwa wakulima ambapo Bodi ya Mazao na Nafaka (NCPB) ililipa wafanyabiashara zaidi ya Sh1.9 bilioni na kuacha wakulima wakiteseka na mpango wa kuwapa wakulima mbolea kwa bei nafuu ambao haujafaulu ulivyopangwa

You can share this post!

Mwamba kurejea nyumbani Nairobi Railway Club ujenzi wa...

Red Star Belgrade yaweka benchi Mkenya Odada ikizidi...