• Nairobi
  • Last Updated May 16th, 2024 8:50 PM
Nakuru yashinda Siaya michuano ya majaribio ya ‘National Deaf Football Trials 2021’

Nakuru yashinda Siaya michuano ya majaribio ya ‘National Deaf Football Trials 2021’

Na RICHARD MAOSI

TIMU ya Nakuru ilianza vyema kampeni ya kujisakia tiketi, ya kushiriki katika Michuano ya Kimataifa ya Olimpiki kwa wale wasiokuwa na uwezo wa kusikiliza na kuongea, itakayofanyika Brazil 2022.

Kipute hicho cha cha siku mbili , kuanzia Alhamisi hadi Ijumaa almaarufu kama, National Deaf Football Trials Cup 2021, kimeleta pamoja timu tano kutoka kaunti za Turkana, Siaya, Nakuru, Kakamega na Kajiado.

Timu ya Nakuru ilikuwa ya kwanza kuingia uwanjani kupambana na Siaya ambapo walishinda 1-0 katika muda wa kawaida.

Licha ya kumiliki asilimia kubwa ya mpira kipindi cha kwanza, Siaya walipoteza nafasi nyingi za wazi.

Nakuru ilipata goli la kipekee kunako dakika ya 15 kupitia mshambuliaji matata Titus Chopkalam ambaye alilemea madifenda wa Siaya na kupiga shuti kali hadi wavuni.

Nakuru nusura waongeze bao la pili dakika ya 72, lakini kipa wa Siaya alilazimika kufanya kazi ya ziada kwa kupangua mikiki iliyokuwa imeelekezwa langoni kipindi cha pili.

Bw Stephen Waweru ambaye ni Mwenyekiti wa Michezo ya Kandanda kwa wasiokuwa na uwezo wa kusikiliza wala kuzungumza aliambia Taifa Leo kuwa michuano hiyo ni ya majaribio kutafuta kikosi ambacho kitawakilisha Kenya katika Michuano ya Afrika.

“Kutoka hapa tutachagua wachezaji bora ambao watajiandaa kutengeneza timu ambayo itawasilisha Kenya katika michuano ya Afrika Mei 2021, na baadaye Olimpiki 2022,” akasema.

Wachezaji wa timu ya Nakuru wakipata tama la maji wakati wa mechi yao dhidi ya Siaya uwanjani Afraha, Nakuru. Picha/ Richard Maosi

Waweru alisema kuwa tayari shirikisho la Kitaifa la Kandanda ya Viziwi (Deaf Football Association of Kenya) walikuwa wamefikia hatua muhimu baada ya kuteua timu ya akina dada mnamo Disemba 2020.

Hata hivyo changamoto kubwa ikiwa ni idadi ndogo ya akina dada ambao hujitokea kucheza kabumbumbu.Aidha ingawa huu ni mchezo wa kitaifa serikali haijajitoeza kugharamia nauli, malazi na marupurupu kwa wachezaji.

“Hivi sasa tunaendelea kufafuta timu mbili za wanaume ambazo zitapeperusha bendera ya taifa,” aliongezea.

You can share this post!

FIFA yampiga Cavani marufuku ya mechi mbili za kimataifa...

Mvua ya mabao Everton wakidengua Tottenham kwenye raundi ya...