• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
FIFA yampiga Cavani marufuku ya mechi mbili za kimataifa kwa kosa la kumchezea vibaya Richarlson wa Brazil

FIFA yampiga Cavani marufuku ya mechi mbili za kimataifa kwa kosa la kumchezea vibaya Richarlson wa Brazil

Na MASHIRIKA

NYOTA Edinson Cavani amepigwa marufuku ya michuano miwili ya kimataifa kwa hatia ya kumkabili visivyo mshambuliaji matata Richarlson Andrade.

Cavani mwenye umri wa miaka 33 alionyeshwa kadi nyekundu katika mchuano wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 ulioshuhudia timu yake ya taifa ya Uruguay ikipokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Brazil mnamo Novemba 2020.

Tukio hilo la dakika ya 71 uwanjani lilimshuhudia Cavani akimkanyaga vibaya Richarlson ambaye ni mwenzake katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kumuumiza kifundo cha mguu.

Uruguay kwa sasa wanajiandaa kwa michuano miwili muhimu ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar ambapo wamepangiwa kuvaana na Argentina kisha Bolivia mwezi ujao wa Machi 2021.

Hata hivyo, Cavani ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Paris Saint-Germain (PSG) na Napoli hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na Uruguay kwenye mechi hizo. Badala yake, Uruguay italazimika kutegemea zaidi huduma za mfumaji wa zamani wa Liverpool na Barcelona, Luis Suarez ambaye kwa sasa anaongoza orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) akivalia jezi za Atletico Madrid.

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limethibitisha kwamba hatia ya Cavani inastahili marufuku ya mechi mbili zijazo za kimataifa.

Mwishoni mwa mechi hiyo ya Novemba, Richarlson alisema angalivunjika mguu kutokana na jinsi ambavyo Cavani alimkabili nay eye aliponea chupuchupu sana.

Habari za kutokuwepo kwa Cavani katika michuano miwili ijayo ya Uruguay zinatarajiwa kumpa kocha Ole Gunnar Solskjaer wa Man-United furaha tele.

Tangu atue ugani Old Trafford bila ada yoyote kutoka PSG, Cavani ushawishi wa Cavani katika safu ya mbele ya Man-United umehisika pakubwa.

Ametikisa nyavu za wapinzani mara sita na kuchangia mabao mengine mawili kwenye kampeni za kuwania ubingwa wa EPL msimu huu. Ukubwa na upekee wa mchango wake umemfanya kuwa na uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Man-United badala ya Anthony Martial ambaye hapo awali alikuwa akishirikiana pakubwa ma Marcus Rashford.

Cavani anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Man-United kitakachovaana na West Bromwich Albion kwenye EPL mnamo Jumamosi ya Februari 13, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wanasoka 6 wa Ganze wafanyiwa majaribio na klabu za Mombasa

Nakuru yashinda Siaya michuano ya majaribio ya...