• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Naomi Osaka katika hatari ya kutozwa faini zaidi na kupigwa marufuku kwenye mashindano ya Grand Slam kwa kususia mahojiano na wanahabari

Naomi Osaka katika hatari ya kutozwa faini zaidi na kupigwa marufuku kwenye mashindano ya Grand Slam kwa kususia mahojiano na wanahabari

Na MASHIRIKA

MWANATENISI nambari moja duniani, Naomi Osaka, sasa anakodolea macho hatari ya kutimuliwa kwenye mashindano ya French Open na kupigwa marufuku kwenye michuano yote ijayo ya Grand Slams iwapo atashikilia msimamo wake wa kususia mahojiano na vyombo vya habari.

Wiki iliyopita, Osaka alisema kwamba hatashiriki mahojiano yoyote wakati wa kipute cha French Open kinachoendelea katika uwanja wa Roland Garros jijini Paris, Ufaransa, ili kumakinikia zaidi afya yake ya akili. Kivumbi hicho kilichoanza Mei 30, kinatarajiwa kutamatika rasmi mnamo Juni 13, 2021.

Osaka alipigwa faini ya Sh1.5 milioni kwa kususia mahojiano na wanahabari mwishoni mwa mechi ya raundi ya kwanza iliyomkutanisha na Patricia Maria Tig wa Romania mnamo Jumapili. Osaka alisajili ushindi wa seti 3-0 za (6-4), (7-6) na (7-4) katika mchuano huo.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na waandalizi wa mapambano manne ya Grand Slam imesema Osaka kwa sasa “amejiweka katika hatari ya kutozwa faini nyinginezo huku akikabiliwa na pigo la kupigwa marufuku kwenye mapambano yajayo ya kuwania mataji ya Grand Slam”.

Katika tukio lililofasiriwa kuwa jibu la moja kwa moja kwa taarifa hiyo, Osaka alitumia mtandao wake wa Twitter kujibu: “Mabadiliko huathiri watu na kuwafanya kutoridhika wala kutulia.”

Baada ya tangazo la Osaka, waandalizi wa French Open walisihi washiriki wote wengine wa kipute hicho kumhimiza mwanatenisi huyo kubadilisha mtazamo wake na kuzingatia kanuni zilizopo. Hata hivyo, juhudi za kumfikia Osaka ziliambulia pakavu.

“Baada ya washiriki wenzake kushindwa kumfikia, waandalizi wa Grand Slam walimwandikia Osaka barua kuhusu uwezekano wake wa kuridhia mpango wa kupokezwa msaada wowote anaohitaji pamoja na kukumbushwa kuhusu majukumu yake,” ikaendelea taarifa hiyo.

Mnamo Jumatano iliyopita, Osaka alitoa taarifa akisisitiza kwamba hatakuwa radhi kuzungumza na wanahabari wakati wote wa mapambano ya French Open akishikilia kwamba mahojiano mengine na vyombo vya habari huathiri pakubwa afya ya akili ya wachezaji.

Kwa mujibu wa kanuni za Grand Slam, mchezaji huwa katika hatari ya kutozwa faini ya hadi Sh2 milioni kwa kususia mahojiano na wanahabari. Kwa upande wao, vinara wa Shirikisho la Tenisi la Wanawake Duniani (WTA) wamesema kwamba “wachezaji wana wajibu wa kuzingatia kanuni zilizopo za kila pambano na kuwatendea haki mashabiki wao.”

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Fainali za Copa America sasa zakosa mwenyeji baada ya...

Nafula aongoza Larissa kunyeshea Asteras AV 10-0 Ligi Kuu...