• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 12:41 PM
Fainali za Copa America sasa zakosa mwenyeji baada ya Argentina pia kupokonywa idhini ya kuziandaa

Fainali za Copa America sasa zakosa mwenyeji baada ya Argentina pia kupokonywa idhini ya kuziandaa

Na MASHIRIKA

KIPUTE cha Copa America 2021 kimesalia bila mwenyeji wiki mbili kabla ya tarehe ambayo fainali hizo zilikuwa zimeratibiwa kuanza.

Hii ni baada ya Argentina kupokonywa idhini ya kuwa mwenyeji wa kinyang’anyiro hicho ambacho walitarajiwa awali kukiandaa kwa pamoja na Colombia.

Colombia walipokonywa haki ya kuandaa fainali hizo mnamo Mei 20, 2021 baada ya kuongezeka kwa visa vya maandamano kutoka kwa raia na wakazi wa taifa hilo waliokuwa wakilalamikia tukio la serikali kuongeza ushuru kwa bidhaa muhimu na za kimsingi.

Shirikisho la Soka la Amerika Kusini (Conmebol) limesema hatua ya Argentina kuzuiwa kuwa mwenyeji wa Copa America imechangiwa na ongezeko la visa vya maambukizi ya virusi vya corona nchini humo.

Pingamizi dhidi ya kuandaliwa kwa fainali za Copa America kwa mara nyingine mwaka huu zimetolewa na wadau wa soka ndani na nje ya serikali ya Argentina.

Mnamo Mei 29, fowadi matata wa Uruguay na klabu ya Atletico Madrid, Luiz Suarez alisema kwamba kinachostahili kupewa kipaumbele na ni afya ya wahusika wakiwemo wachezaji na mashabiki.

Conmebol wamesisitiza kwamba kwa sasa wanatathmini hali ya maambukizi ya corona katika mataifa mengine yatakayofichua azma ya kuwa wenyeji wa kipute hicho kinachojumuisha vikosi 10.

Fainali za Copa America mwaka huu wa 2021 zilikuwa zimeratibiwa kufanyika kati ya Juni 13 na Julai 10. Kipute hicho hakikufanyika mnamo 2020 kwa sababu ya janga la corona. Brazil ndio mabingwa watetezi wa kivumbi hicho baada ya kutawazwa mabingwa mnamo 2019.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

DIMBA MASHINANI: Kigogo mchezo wa jadi usiobagua umri, hadhi

Naomi Osaka katika hatari ya kutozwa faini zaidi na kupigwa...