• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
Nilipoteza kilo nne nilipougua malaria baada ya kuchezea Gabon kwenye AFCON – Aubameyang

Nilipoteza kilo nne nilipougua malaria baada ya kuchezea Gabon kwenye AFCON – Aubameyang

Na MASHIRIKA

FOWADI na nahodha wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang, amesema kwamba alipunguza jumla ya kilo nne na akawa dhaifu zaidi kwa siku kadhaa baada ya kuugua malaria wakati akiwakilisha timu yake ya Gabon kwenye mechi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) mnamo Machi 2021.

Aubameyang, 31, alirejea ugani katika kipindi cha pili kuwajibikia Arsenal mnamo Aprili 29, 2021 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa Europa League ulioshuhudia waajiri wake wakipokezwa kichapo cha 2-1 dhidi ya Villarreal ya kocha Unai Emery nchini Uhispania.

“Hicho kilikuwa kipindi kigumu zaidi kwangu. Sijawahi kuugua namna hiyo maishani mwangu. Nilikuwa nikijihisi vibaya sana na mwili mzima ukanyong’onyea. Nilikuwa katika hali mbaya,” akasema Aubameyang.

Fowadi huyo aliyefunga bao katika ushindi wa 3-0 uliosajiliwa na Gabon dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwenye gozi la kufuzu kwa fainali za AFCON mnamo Machi 25, alisema kwamba alianza kujihisi vibaya wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowakutanisha Arsenal na Liverpool uwanjani Emirates mnamo Aprili 3, 2021.

“Safari ya kutoka Uingereza hadi Gabon na kurudi si rahisi kwa sababu ya umbali. Nilijihisi mchovu wakati wa mechi dhidi ya Liverpool. Mwanzo nilidhani ni uchovu na mavune tu ya kusafiri,” akatanguliza nyota huyo wa zamani wa Borussia Dortmund.

“Nilihisi joto kwa siku tatu mfululizo usiku na mchana bila kukoma. Nilimeza dawa aina za paracetamol lakini sikupata nafuu. Baada ya hapo, nilitafuta huduma za daktari aliyegundua kwamba nilikuwa naugua malaria.”

“Nililazwa hospitalini kwa siku tatu na nilikuwa katika hali mbaya. Nilipoteza jumla ya kilo nne,” akaeleza.

Baada ya kuchezea Arsenal kwenye mkondo wa kwanza wa robo-fainali za Europa League dhidi ya Slavia Prague mnamo Aprili 8, 2021, Aubameyang alikosa marudiano ya kipute hicho na mechi tatu nyingine zilizosakatwa na Arsenal kwenye EPL.

Alipangwa kwenye kikosi cha kwanza kilichotegemewa na kocha Mikel Arteta dhidi ya Newcastle United katika uga wa St James’ Park mnamo Mei 2, 2021, na akafunga bao na kuchangia jingine katika ushindi wa 2-0 waliousajili kwenye mchuano huo wa ligi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

FAUSTINE NGILA: Serikali isikimye gharama ya intaneti...

Uhuru, Raila wataka wabunge na maseneta kupitisha mswada wa...