• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Nilitarajia Messi atoe ombi la kuchezea Barcelona bila kudai malipo – Laporta

Nilitarajia Messi atoe ombi la kuchezea Barcelona bila kudai malipo – Laporta

Na MASHIRIKA

RAIS wa Barcelona Joan Laporta amesema alitarajia fowadi Lionel Messi angesalia uwanjani Camp Nou na kuhiari kuchezea miamba hao wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) bila kutaka kulipwa ada yoyote.

Messi, 34, aliagana na Barcelona mnamo Agosti 2021 na kuyoyomea Ufaransa kuvalia jezi za Paris Saint-Germain (PSG). Hii ni baada ya Barcelona kushindwa kumpa mkataba mpya kutokana na kanuni zinazodhibiti kiasi cha mishahara ya wanasoka wa La Liga.

Messi aliyeongoza Barcelona kunyanyua mataji 10 ya La Liga, alilazimika kuondoka licha ya kupendekezea Barcelona kumpa ofa mpya yenye mshahara uliopunguzwa kwa asilimia 50.

“Kulikuwa na masikitiko makubwa kwa pande zote mbili. Nilidhani Messi angekubali kuchezea Barcelona bila kutarajia malipo yoyote. Vinara wa La Liga wangekubali mpangilio huo. Lakini tena ni vigumu kumsihi mchezaji wa kiwango cha Messi kufanya mambo kama hayo,” akasema Laporta katika mahojiano yake na kituo cha redio cha RAC mjini Catalonia, Uhispania.

Laporta alitumia mahojiano hayo kama jukwaa la kufafanua kuhusu jinsi ambavyo mpango wa kumpa Messi kandarasi mpya ungeweka Barcelona katika “hatari kubwa” kiuchumi.

Tangu Messi abanduke Camp Nou, makali ya Barcelona yameshuka pakubwa japo Laporta ameshikilia kwamba ataendelea kumuunga mkono kocha Ronald Koeman.

“Nilimuuliza Koeman iwapo ana imani na timu yake na akanieleza kwamba cha pekee anachohitaji kuona kwa sasa ni wanasoka wanaouguza majeraha wakirejea ulingoni kwa wakati kabla ya ufufuo wa makali ya Barcelona kuonekana,” akasema.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Jamhuri ya Ireland yapepeta Azerbaijan na kusajili ushindi...

Kaunti za Pwani kusaka ?watalii kama eneo moja