• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Nondies kwenye mizani ya Strathmore ligi ya raga ikiingia wiki ya tatu

Nondies kwenye mizani ya Strathmore ligi ya raga ikiingia wiki ya tatu

Na AYUMBA AYODI

KLABU inayojivunia mataji mengi ya Ligi Kuu ya Raga nchini (Kenya Cup) Nondescripts itaanza kampeni yake ya msimu huu kwa kualika Strathmore Leos saa saba mchana uwanjani RFUEA hapo Jumamosi.

Uga huo pia utatumiwa kwa mchuano mwingine kati ya wenyeji Kenya Harlequin na mabingwa Sisimuka Charity Cup Kabras Sugar saa tisa alasiri, huku uwanja wa KCB Ruaraka ukiandaa michuano mingine miwili.

Wanabenki wa KCB, ambao wanatetea taji baada ya Kenya Cup ya msimu uliopita kufutiliwa mbali, watakaribisha Blak Blad kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta saa saba mchana kabla ya Mwamba kuwa mwenyeji wa Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST) saa mbili baadaye.

Menengai Oilers, ambao walirukia uongozi baada ya michuano ya raundi ya tatu kwa mara ya kwanza kabisa, wataalika Impala Saracens uwanjani ASK Nakuru saa saba mchana.

Nakuru watapumzika Jumamosi.

Nondies, ambao wanawinda kushinda ligi kwa mara ya 18, lakini ya kwanza tangu 1998, wanatarajiwa kusumbuliwa na kutokuwa tayari wanapokabiliana na wanafunzi wa Leos ambao tayari wameshamenyana na miamba.

Leos walikaribia kuduwaza KCB katika raundi ya kwanza ambayo wanabenki walitoka nyuma na kutawala 24-16.

Vijana wa kocha Louis Kisia kisha walipoteza dhidi ya mabingwa wa mwaka 2016 Kabras 35-9 katika raundi ya pili kabla ya kupumzika wikendi iliyopita.

Licha ya vichapo hivyo, Leos wameonyesha wana uwezo na wako tayari kwa kibarua mbele yao baada ya kupandishwa ngazi msimu huu. Ni muda tu kabla ya Leos waandikishe ushindi wao wa kwanza.

Kwa sasa haijulikani kama Leos wanaweza kuzima ‘simba wekundu’ Nondies ambao wameimarisha kikosi kwa kununua Charles Omondi kutoka Homeboyz, Fidens Tony (Northern Suburbs), Kariuki Kanyiri (Strathmore Leos), Brian Omondi (Northern Suburbs) na Samuel Motari (Impala Saracens).

“Tumefanya kile tunaweza na tunatumai mpira utatupenda,” alisema kocha wa Nondies, Willis Ojal na kuongeza kuwa Leos wameshapata kucheza mechi kadhaa kwa hivyo wamepata uzoefu wa mechi.

“Lakini naamini mpango wetu utaweza kutupa matokeo mazuri,” alieleza Ojal ambaye alifichua kuwa uwanja wao wa farasi wa Ngong Racecourse sasa uko tayari, ukisubiri kukaguliwa na Shirikisho la Raga nchini (KRU).

Nondies imehama kutoka uwanja wa kilimo wa Jamhuri Park, ambao imekuwa ikitumia kwa miaka 20. Ojal anatumai kuwa mabadiliko ya uwanja yatakuwa na baraka.

“Hatua hii ni sawa na kutimiza sehemu ya azma yetu ya kushinda mataji makubwa. Uwanja wetu mpya na mazingira ni vitu vizuri kwa wachezaji na makocha. Tutakuwa na udhibiti zaidi wa eneo hilo,” alisema Ojal.

Quins ilizoa ushindi wake wa kwanza msimu huu kwa kupepeta majirani na mahasimu wakuu Impala 27-20 katika gozi la Ngong Road. Ilikuwa imenyukwa 39-13 katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Menengai Oilers kabla ya kupoteza pembamba 35-32 wikendi iliyopita.

Wanasukari wa Kabras walifyeka MMUST 56-0 na Strathmore 35-9 katika mechi zao mbili za kwanza.

KCB imezoa ushindi mwembamba mara mbili – dhidi ya Leos na Quins – nayo Blak Blad iliandikisha ushindi wa kwanza juma lililopita kwa kunyamazisha Mwamba 24-17. Blak Blad ilikuwa imepoteza 13-8 dhidi ya Top Fry Nakuru kabla ya kutoka sare ya 12-12 dhidi ya Menengai Oilers.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

Rais Suluhu awahimiza Watanzania kuungana

Mganda Wadri na raia wa Rwanda Mbungo wafagia tuzo bora za...