• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
Omanyala akiuka kisiki, asema atafana Amerika

Omanyala akiuka kisiki, asema atafana Amerika

NA GEOFFREY ANENE

NYOTA Ferdinand Omanyala ametuliza nyoyo za Wakenya baada ya hatimaye kusafiri kuelekea Amerika, Alhamisi kukurupuka mbio za mita 100 katika Riadha za Dunia.

Mshikilizi huyo wa rekodi ya Afrika alisema hakuna aliyekuwa na njama ya kumfungia nje katika riadha hizo zinazoanza mjini Oregon jimboni Oregon, Amerika, Ijumaa usiku, kwa siku 10.

Akiwa mwingi wa ghera na ari baada ya kupata viza ya kusafiri hadi Amerika Alhamisi adhuhuri kufuatia Wakenya kukosoa vikali Ubalozi wa Amerika jijini Nairobi, Waziri wa Michezo, Amina Mohamed na Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki Kenya (NOC-K). Omanyala alisema kuwa hakuna wa kulaumiwa.

Wakenya waliojaa hasira walirushia ubalozi huo, Waziri na NOC-K maneno makali baada ya kupokea habari kuwa Omanyala sasa hatashiriki mashindano hayo yaliyovutia zaidi ya wanariadha 1,900 kutoka mataifa 192 kwa sababu viza yake haikuwa tayari, siku moja tu kabla ya bastola ya kuanza mashindano kulia.

Walilaumu Amerika kwa kula njama ya kuhakikisha watimkaji wake hawapati ushindani mkali kutoka kwa bingwa huyo wa Afrika anayeshikilia pia rekodi ya Afrika ya sekunde 9.77, muda ambao ni wa nane-bora katika historia.

Bingwa huyo wa Kip Keino Classic anajivunia muda wa tatu-bora mwaka huu wa sekunde 9.85, nyuma ya Waamerika Fred Kerley (9.76) na mshindi wa Kip Keino Classic 2021 Trayvon Brommel (9.81).

Aliratibiwa kusafiri hadi Oregon saa kumi na mbili jioni jana na kuwasili saa mbili na dakika 40 kabla ya kujibwaga uwanjani Hayward Field.

Alifaa kuwa Mkenya wa kwanza kutifua vumbi kabla ya mabingwa wa Afrika kushiriki matembezi ya kasi kwa mwendo wa kilomita 20; Emily Ngii na Samuel Gathimba, na bingwa mara mbili wa mbio za kuruka viunzi na maji mita 3,000 Conseslus Kipruto pamoja na Benjamin Kigen, Leonard Bett na Abraham Kibiwot.

Judith Kiyeng, Winny Chebet, Edinah Jebitok na bingwa wa Olimpiki, Faith Kipyegon watakimbia mita 1,500 kabla ya Omanyala kushiriki robo-fainali iwapo atatimiza muda unaohitajika katika raundi ya kwanza.

Alishukuru kila aliyempigania kupata viza akitetea Ubalozi wa Amerika aliposema ulifuata taratibu zake.

Pia, alisema Waziri Amina alifanya kila juhudi kuhakikisha amepata viza hiyo. Isitoshe, alimshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kuingilia kati pamoja na Shirikisho la Riadha Kenya kwa kumtafutia ndege. Aliwataka Wakenya wawe na mtazamo mzuri akisema ana mshawasha licha ya kuwa atajibwaga uwanjani Ijumaa, siku ya kuwasili kwake.

“Ninaomba nifike Eugene kwa muda ufaao na Mungu akinipatia nguvu nidhibiti presha niliyonayo… Nimekuwa nikifanya mazoezi kwa mwaka mzima na niko tayari. Ni kufa-kupona kwangu kwenye mbio hizo kwa hivyo ni muhimu. Ni changamoto nimwekewa mezani ambayo ni lazima niikabili uso kwa macho. Sina tashwishi ubalozi ulinipa visa kwa moyo mmoja,” aliongeza.

Baadhi ya wanariadha watajika waliokashifu utata huo wa viza kwa washiriki ni pamoja na raia wa Ivory Coast Marie-Jose Ta Lou aliyesema, “Inasikitisha kuona wanariadha wanafanya kazi kubwa ya kufuzu halafu wanakumbwa na matatizo ya kupata visa ya kusafiri”.

Bingwa wa zamani wa Olimpiki na Dunia mbio fupi Michael Johnson pia alikosoa ucheleweshaji huo.

  • Tags

You can share this post!

Wanahabari wengi wanahofia kuhudhuria kampeni za Ruto...

Jubilee yakopa Sh300 bilioni inapojiandaa kuondoka mamlakani

T L