• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
PSG wasema Mbappe si wa kung’olewa jijini Paris hivi karibuni

PSG wasema Mbappe si wa kung’olewa jijini Paris hivi karibuni

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

MIAMBA wa soka ya Ufaransa, Paris Saint-Germain (PSG), wamesisitiza kwamba nyota Kylian Mbappe atasalia ugani Parc des Princes msimu ujao licha ya huduma za fowadi huyo raia wa Ufaransa kuhemewa na Real Madrid ya Uhispania.

Mbappe, 22, aliwafungia PSG jumla ya mabao 42 katika mapambano yote ya msimu wa 2020-21. Mkataba wa sasa kati ya PSG na sogora huyo wa zamani wa AS Monaco unatamatika rasmi mnamo Juni 2022.

“Mbappe haendi popote. Ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha PSG. Hatuna mpango wowote wa kumtia mnadani hivi karibuni na hataondoka kambini mwetu bila ada yoyote. Isitoshe, anapata kila kitu anachohitaji hapa Paris,” akatanguliza rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi.

“Ataondoka aende wapi? Ni kikosi kipi kwa sasa, katika kigezo cha kukuza wachezaji kitaaluma, kina uwezo wa kushindana na PSG? Ninachoweza kusema ni kwamba mambo ya Mbappe yako sawa na matarajio yetu ni kwamba atarefusha mkataba wake nasi.”

“Hapa ni Paris. Hili ni taifa lake. Ana maazimio ya kuendelea kusakata kabumbu, kuvumisha Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1), nchi yake na jiji kuu la Paris,” akaongeza kinara huyo katika mahojiano yake na gazeti la L’Equipe nchini Ufaransa.

PSG walikamilisha kampeni za muhula wa 2020-21 wakijivunia taji moja pekee la French Cup. Waliambulia nafasi ya pili kwenye Ligue 1 nyuma ya Lille waliowazidi kwa alama moja pekee na wakabanduliwa na Manchester City kwenye nusu-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Mnamo 2019, Al-Khelaifi pia alisema kwamba Neymar hakuwa na nia ya kurejea Barcelona miaka miwili baada ya kuondoka Uhispania na kutua Ufaransa.

“Barcelona walitaka sana kumrejesha Neymar ugani Camp Nou. Si siri. Lakini je, Neymar alifaulu kurudi? Hapana.”

“Ni kweli kwamba ilichukua muda mrefu kabla ya azoee maisha ya Ufaransa lakini hata ukimpigia simu leo atakwambia jinsi anavyoridhika na kufurahia maisha yake jijini Paris,” akasema Al-Khelaifi.

 

You can share this post!

Aston Villa wajinasia huduma za kiungo Buendia kwa Sh4.6...

Kenya Lionesses haijapata mwangaza kutoka Wizara ya Michezo...