• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Kenya Lionesses haijapata mwangaza kutoka Wizara ya Michezo kuanza kambi ya mpira wa vikapu

Kenya Lionesses haijapata mwangaza kutoka Wizara ya Michezo kuanza kambi ya mpira wa vikapu

Na GEOFFREY ANENE

KENYA Lionesses inasubiri mwelekeo kutoka kwa Wizara ya Michezo kabla ya kuingia kambini kwa mashindano ya Ukanda wa Tano ya mpira wa vikapu ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AfroBasket).

Vipusa hao wa kocha George Mayienga wamekuwa wakifanya mazoezi ya siku nzima wikendi pekee. Mazoezi ya siku nyingine za juma yamekuwa ni jioni. Yamekuwa katika ukumbi wa kitaifa wa Nyayo.

“Tunafanya mipango ya kuanza kufanya mazoezi siku nzima kuanzia Jumatano (kesho). Bado tunasubiri mwelekeo kutoka kwa Wizara ya Michezo kabla ya kufanya hivyo kwa sababu tutahitaji kuishi mahali pamoja,” mratibu wa mazoezi ya timu hiyo Angela Luchivya alieleza Taifa Leo hapo jana.

Naibu huyo wa katibu wa Shirikisho la Mpira wa Vikapu Kenya (KBF) aliongeza kuwa kambi ya Lionesses itakuwa na wachezaji wote kufikia wikendi inayokuja. “Tunatarajia wachezaji wetu wa kimataifa waliobaki kufikia mwishoni mwa juma.

Klabu anayochezea Georgia Adhiambo nchini Rwanda inapanga kumuachilia Jumatano nao Rose Ouma (Milki za Kiarabu) na Brenda Adhiambo na Purity Auma (Amerika) watakuwa hapa kufikia wikendi,” alisema nyota huyo wa zamani wa Lionesses.

Felmas Koranga (Amerika), Mercy Wanyama (Uhispania) na Victoria Reynolds (Amerika) walijiunga na wachezaji wanaocheza humu nchini zaidi ya wiki moja iliyopita. Naye Mayienga aliwasili Ijumaa kutoka Uganda anakotia makali klabu ya wanaume na pia wanawake ya JKL Dolphins.

Mashindano ya Ukanda wa Tano yanatarajia kuvutia Kenya, Rwanda, Uganda, Burundi, Tanzania, Somalia na wenyeji na mabingwa watetezi Misri. Kuna uwezekano yatatumia mfumo wa mzunguko. Mshindi ataingia AfroBasket.

You can share this post!

PSG wasema Mbappe si wa kung’olewa jijini Paris hivi...

Kiungo na nahodha wa Ghana, Andre Ayew, kuagana na Swansea...